Kikosi cha Pauni 930 mil hiki hapa

Wednesday September 16 2020

 

LONDON, ENGLAND. LIGI Kuu England imeshaanza huku kikipangwa kikosi matata kabisa cha mastaa wenye thamani kubwa sokoni ambao watapiga mzigo kwenye mikikimikiki ya ligi ya kibabe.

Kwa mujibu wa Transfermarkt, kikosi hicho kina thamani ya Pauni 930 milioni na kuhusisha mastaa kibao wenye majina makubwa kwenye ligi hiyo.

Kikosi chenyewe, golini kipa ni Alisson Becker ambaye ametajwa kuwa na thamani ya Pauni 64 milioni akiwapiku Ederson na David De Gea kwenye nafasi hiyo.

Kwenye safu ya mabeki wapo Virgil Van Dijk (Pauni 72 milioni) ambaye anaungana na Andrew Robertson (Pauni 57.6 milioni), Trent Alexander-Arnold (Pauni 99 milioni) na Aymeric Laporte (Pauni 54 milioni). Kikosi hicho hakina nafasi ya wachezaji Harry Maguire, Davinson Sanchez na Ben Chilwell licha ya kwamba walisajiliwa kwa pesa ndefu.

Kwenye sehemu ya kiungo N’Golo Kante anapata nafasi akithaminishwa kuwa na thamani ya Pauni 72 milioni sawa na Mfaransa mwanzake, Paul Pogba huku Kevin de Bruyne akikamilisha safu hiyo ya kiungo akiwa na thamani ya Pauni 108 milioni sokoni na kuwaweka kando Kai Havertz, Bruno Fernandes na Dele Alli.

Kwenye fowadi yupo Raheem Sterling mwenye thamani ya Pauni 115.2 milioni, Mohamed Salah (Pauni 108 milioni) na mshambuliaji wa kati ni Harry Kane, ambaye ametajwa kuwa na thamani ya Pauni 108 milioni kwa mujibu wa Transfermarkt.

Advertisement

Kikosi hicho kinashuhudia mastaa kibao wakikosa namba kama vile Roberto Firmino, Timo Werner, Anthony Martial na Pierre-Emerick Aubameyang - ambaye anathaminishwa kuwa na thamani ya Pauni 50 milioni.

Advertisement