Kiduku aonywa

Wednesday October 28 2020
kiduku pic

Dar es Salaam. Wakati mashabiki wa ndondi nchini wakihesabu siku kushuhudia pambano la ubingwa wa mabara la WBC kati ya Twaha ‘Kiduku’ Kassim na Sirimongkhon Iamthuam ‘Sirimongkol Singwancha’ wa Thailand, bondia nyota wa zamani, Mbwana Matumla amempa mbinu Kiduku.

Kiduku na Singwancha watacheza pambano la raundi 10 la uzani wa super middle litakalofanyika kwenye Ukumbi wa PTA, Sabasaba, Dar es Salaam.

Awali, mabondia hao walitarajiwa kukutana uso kwa uso jana, lakini Twaha aliomba zoezi hilo lisogezwe hadi kesho ili apate muda wa kupiga kura leo mjini Morogoro, na sasa watapima uzito na afya kesho.

Twaha atamkabili Mthailand akiwa amemzidi ubora kwani Mtanzania huyo ni bondia wa nyota 2.5 na Sirimongkol ana nyota 1.5 ingawa amemshinda uzoefu Kiduku, kwani amepigana mapambano 97, ameshinda KO mara 62 na kupigwa mara nne. Kiduku amecheza mapambano 22, ameshinda 15, manane kwa KO, amepigwa 6.

“Akitaka kushinda pambano Kiduku asishindane naye, kwani Wathailand ni mabondia wanaolazimisha ili kupata matokeo,” alisema Mbwana.

Alisema Kiduku anapaswa kushambulia na kutoka.

Advertisement

“Acheze huku anatembea, akishambulia sekunde 20 anatoka, akicheza hivyo hata KO atampiga Mthailand,” alisema Mbwana akitolea mfano wa pambano lake alilowahi kuzichapa na Mfilipino.

“Mfilipino alikuwa hatari, ila nilimpiga KO hakuamini, wamekuwa wakitusoma na kujua uchezaji wetu, hata Kiduku itakuwa ni hivyo ila Ijumaa abadilike,” alisema.

Kiduku, ambaye amepiga kambi Mazimbu, Morogoro amesisitiza kuwa fiti na kuwaahidi Watanzania kubakisha taji hilo nchini.

“Niko fiti, nimejiandaa na sitarajii kuachia ubingwa huu uondoke nchini, ni fursa ambayo imekuja nyumbani,” alisisitiza Kiduku.

Pambno hilo litatanguliwa na mengine sita. Alphonce Mchumiatumbo atacheza na Jongo Jongo, Maono Ally atazichapa na Joseoh Sinkala, Ibrahim Tamba (Tamba uone) atacheza na Said Juma.

Francis Miyeyusho ‘Chichi Mawe’ atacheza na Said Wigo, Hamza Iddy atacheza na Jamal Kunoga na Ruth Chisale atacheza na Sijali Said upande wa wanawake.

 

Advertisement