Kaze ni kazi kazi leo Uhuru

Muktasari:

Huu ni mchezo wa kwanza wa Kaze kama kocha wa Yanga.

 

Dar es Salaam. Kocha Cedric Kaze anashusha kikosi chake cha kwanza leo dhidi ya Polisi Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kaze raia wa Burundi amefanya kazi na Yanga kwa takribani wiki moja tangu alipowasili kuchukua mikoba ya Zlatko Krmpotic, wakati macho na masikio ya wanachama na mashabiki wa timu hiyo wakiwa na shauku ya kutaka kuona mabadiliko.

Katika mazoezi ya muda mfupu ambao Kaze ameyaongoza tangu alipotua nchini, ni wazi kuwa alitaka kuwa na mfumo ambao utatengeneza nafasi nyingi za kufunga tofauti na ilivyokuwa awali.

Gazeti hili lilimshuhudia Kaze akifanya kazi ya kuwaleta pamoja wachezaji wote wa kikosi cha kwanza na wale ambao walikuwa hawatumiki ili kuwapa nafasi upya ya kuingia katika kikosi chake cha kwanza.

Kocha huyo alionekana akizungumza kwa muda na Waziri Junior, ambaye hajapata nafasi ya kuichezea Yanga hata mechi moja ya Ligi Kuu Tanzania Bara tangu aliposajiliwa akitokea Mbao FC iliyoshuka daraja.

Mazungumzo ya Kaze pia yaliwahusu Haruna Niyonzima, lakini baada ya mazoezi aliwaita pembeni Deus Kaseke, Lamine Moro na Zawadi Mauya.

Kaze mwenye miaka 40 alisema lengo lake kuzungumza na wachezaji ni kuleta timu pamoja na kila mchezaji kujiona ana umuhimu katika kikosi chake.

“Ni kawaida yangu kusema na wachezaji mawili matatu kabla na baada ya mazoezi, lengo langu nataka kila mchezaji ajione ni sehemu ya timu, asiwepo wakujisikia thamani yake ni ndogo kuliko mwingine, hilo naamini litazaa umoja wenye nguvu ya kufanya vitu kwa pamoja na vikatimia,” alisema.

Katika mchezo wa leo, kocha huyo alisema tayari ana kikosi cha kwanza kwa muda mfupi aliokaa na timu na anaamini kinaweza kufanya vizuri huku akiendelea kufanya maboresho.

“Nimeendelea kuwasoma wachezaji katika mazoezi yanayofanywa kila siku, nimeanza kukiona kikosi cha kwanza, ndiyo maana kabla ya yote nilitamani kila mchezaji ajione ndani ya kikosi ili asiwepo wa kuona majukumu yake si muhimu,” aliongeza.

Kwa upande wao, Polisi Tanzania, ambao walikuwa na mazoezi ya mwisho jana kwenye Uwanja wa Uhuru, wanaamini mchezo utakuwa mgumu, lakini mipango yao ni kuibuka na pointi tatu.

Kocha wa Polisi, Ally Suleiman Mtuli alisema timu yake haina presha na mchezo huo na wamejiandaa kushinda.

“Kwenye soka hakuna timu kubwa, tunaiheshimu Yanga kama timu kongwe nchini, lakini tulichokifuata ni ushindi na anaamini tutashinda mchezo wetu,” alisema Mtuli.

Yanga na Polisi zimekuwa timu ngumu kufungana katika michezo miwili iliyopita ya Ligi Kuu Tanzania Bara, wakati mchezo wa kwanza wa msimu uliopita, mshambuliaji wa sasa wa Yanga akiwa Polisi, Betram Nchimbi aliwafunga waajiri wake wa sasa mabao yote matatu katika sare ya 3-3.

Katika mchezo wa marudiano uliofanyika Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, zilitoka sare ya bao 1-1, bao la Yanga likifungwa na Tariq Seif, ambaye sasa anaichezea Polisi Tanzania.

Yanga inashuka katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union, mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Oktoba 3.

Polisi Tanzania, ambao mchezo wa leo unakuwa wa saba katika msimamo wa Ligi Kuu, inashuka kwenye Uwanja wa Uhuru ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Gwambina, mchezo uliofanyika Jumatatu mjini Moshi.

Hadi sasa, Yanga imecheza michezo mitano, ikishinda minne na sare moja na kukaa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, huku Polisi Tanzania ikiwa imecheza mechi sita, ikishinda mechi tatu, sare mbili na kufungwa mchezo mmoja. Inashika nafasi ya saba ikiwa na ukuta imara ulioruhusu mabao matatu pekee.