Saliboko amekubali unyonge KMC

Muktasari:
- Saliboko aliyewahi kung’ara msimu wa 2019/20 akifunga mabao 12 akiwa na Lipuli ya mjini Iringa, alisema kitendo cha msimu huu kupitia changamoto ya majeraha kilimfunza kujua namna ya kukabiliana na nyakati ngumu ili kuhakikisha hazimuondoi mchezoni.
MSHAMBULIAJI wa KMC, Daruweshi Saliboko amesema japo hakuwa na msimu mzuri kiushindani haujapita kapa badala yake amepata mafunzo yatakayomsaidia ujao kufanya vizuri katika kuweka rekodi za heshima.
Saliboko aliyewahi kung’ara msimu wa 2019/20 akifunga mabao 12 akiwa na Lipuli ya mjini Iringa, alisema kitendo cha msimu huu kupitia changamoto ya majeraha kilimfunza kujua namna ya kukabiliana na nyakati ngumu ili kuhakikisha hazimuondoi mchezoni.
“Mchezaji unapopitia magumu kama unakuwa haupo imara kukabiliana nayo ni rahisi kuondoka katika mstari. Hilo linatokana na kulitegemea soka kuwa chanzo kikuu cha kipato chetu,” alisema Saliboko na kuongeza:
“Jambo kubwa nililokuwa najifunza licha ya kukaa nje kwa muda mrefu nilitumia muda wangu kuzingatia matibabu, kutazama mechi walizokuwa wanacheza wengine na kurudia zile ambazo nilicheza ili kujua kipi nikifanyie kazi zaidi. Baada ya kupona nikaanza mazoezi kwa bidii.
“Katika mechi chache nilizocheza msimu huu nimefunga mabao mabao mawili na asisti mbili, msimu uliopita nilimaliza na mabao manne na asisti tatu, hivyo najipanga msimu ujao kuwa na namna kubwa zitakazofanya thamani yangu kupanda.”
Saliboko alisema kitu kikubwa anachokitamani ni kuona anakuwa na muendelezo na kiwango chake kama ilivyo kwa baadhi ya wachezaji wazawa ambao wamekuwa wakifanya vizuri kwa mfululizo.
“Mfano anachokifanya Feisal Salum ‘Fei Toto’ msimu uliopita alikuwa anachuana kufunga mabao mengi na Aziz Ki na msimu huu ndiye kinara wa asisti 13 na mabao manne, bila kupepesa macho anastahili kutiwa moyo ili azidi kusonga mbele kama mzawa,” alisema mchezaji huyo.