Kaze: Anzeni kuhesabu!

KOCHA mpya wa Yanga, Cedric Kaze amewaambia mashabiki kwamba amesikia shangwe zao baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania, sasa ameahidi kuwapa furaha zaidi kwani ndiyo kwanza ameanza.

Hiyo ilikuwa ni mechi yake ya kwanza tangu afanye mazoezi ya wiki moja na kesho Jumapili atakuwa Mwanza kuikabili KMC ndani ya CCM Kirumba.

Kaze aliiambia Mwanaspoti kwamba: “Ndiyo kwanza tumeanza, mambo mazuri yanakuja.”

Kocha huyo amesisitiza kwamba mkakati wake namba moja ni kupangua mchezo mmoja baada ya mwingine na amewataka wachezaji kila mchezo wacheze kama fainali kwani mchuano ni mkali.

Alisema amefurahia kiwango na aina ya uchezaji walioanza nao wachezaji wake, lakini anahitaji kufanyia kazi zaidi pasi za mwisho, umiliki wa mpira na kuurejesha mpira ukishaporwa na kucheza kwa kasi. “Nataka kuona kila mmoja anapiga pasi na kumiliki mpira kuanzia nyuma mpaka eneo la timu pinzani.”

Alisema: “Hata kama tutakuwa tunacheza na timu ambayo inatukaba katika eneo letu, sitaki kuona mchezaji wangu anabutua mpira, nataka kuona tunapiga pasi kuanzia katika eneo letu mpaka kufika kwao na kama ikitokea kubutua basi iwe mahala kwenye ulazima wa kufanya hivyo.

“Ukiangalia katika mechi tano ambazo zimepita Yanga walizocheza kwenye ligi bila uwepo wangu ni tofauti kabisa na mpira ambao tulicheza na Polisi Tanzania licha ya ubora wao na uwezo wa kukaba tulimiliki mpira na kupiga pasi kuanzia nyuma mpaka kufika kwao na tukafanikiwa kupata bao.”

Kwa mujibu wa rekodi Yanga na Azam hazijapoteza mchezo wowote huku kipa Metacha Mnata akiwa hajaruhusu bao tangu ligi kuanza.

 

MECHI YA KWANZA

Katika mtihani huo wa kwanza wa Kaze, Yanga ilionekana tofauti kwa kuanzia mashambulizi nyuma.

 

FARID, NIYONZIMA WAREJEA

Kwenye kikosi cha juzi, Kaze alifanya mabadiliko machache katika kikosi cha kwanza na kumrudisha kikosini winga wa kushoto, Farid Mussa sambamba na kiungo mkongwe Haruna Niyonzima. Nyota hao hawakuwa wanaanza katika utawala wa kocha Krmpotic aliyetimuliwa, hakupangua safu ya ulinzi aliwaacha kipa Metacha, beki wa kulia Kibwana Shomari, beki wa kushoto Mustapha Yassin na mabeki wa kati nahodha Lamine Moro na Bakari Mwamnyeto.

Safu ya kiungo Mukoko Tonombe na Feisal Salum waliendelea kupewa nafasi ambapo waliungana na Niyonzima.

Wengine ni pamoja na winga Tuisila Kisinda na Farid Mussa ambao walishambulia wakitokea pembeni na mbele alianza Yacouba Sogne. Katika mchezo huo, Farid ambaye alihusika katika upatikanaji wa bao la Yanga lililofungwa na Tonombe alionekana kuwa kwenye kiwango bora, huku Niyonzima akiwa na majukumu mapya kikosini.

 

JUKUMU LA NIYONZIMA

Niyonzima ambaye alikuwa akicheza kama kiungo mshambuliaji alikuwa anaamua muda gani timu ishambulie na upi izuie sambamba na kuhakikisha anakuwepo eneo lolote ambalo mpira utakuwapo bila kujali upo kwa timu pinzani au upande wao.

Kwa zaidi ya asilimia 60, Niyonzima alionekana kuyatimiza majukumu hayo ingawa kasi yake ilionekana kupungua kipindi cha pili ndipo Kaze alipoamua kumfanyia mabadiliko na kuingia Ditram Nchimbi aliyekuwa akitokea pembeni huku ikibidi Farid kutekeleza kile ambacho alikuwa akikifanya Mnyarwanda huyo.

Awali, Niyonzima alikuwa akitumika kama kiungo wa pembeni na hata alipocheza kama kiungo mshambuliaji hakuwa akipewa uhuru wa kuzunguka.

 

MASHAMBULIZI

Yanga ilikuwa tofauti kwenye namna ya kutengeneza mashambulizi, alionekana Metacha kuyaanzisha nyuma na kusogea taratibu huku hesabu zikibadilika pindi wavukapo mstari wa kati. Namna hiyo ya kuanzisha mashambulizi ilikuwa ikiwavuta wapinzani wao na kusogea juu kupokonya mipira kitu ambacho kilikuwa kikiwapa urahisi viungo wa Yanga kupokea mipira wakiwa huru kutokana na wachezaji ambao walivutika wakati shambulizi likianzishwa.

 

YANGA BILA MPIRA

Yanga walipokuwa hawana mpira aliyeonekana kuwa mtu wa kwanza kuutafuta alikuwa mshambuliaji wa mwisho huku akipewa usaidizi na kiungo mchezaji kwa sasa wanaonekana kukabia juu.

Kila ambapo Yanga walionekana kupoteza mpira waliutafuta kwa nguvu.

Miongoni mwa maeneo ambayo yanaonekana kumuangusha Kaze na mbinu yake ya kucheza mpira wa chini unaochagizwa na pasi fupifupi kuelekea eneo la adui ni la golikipa ambapo katika mchezo huo alianza na Metacha ambaye hakuonyesha ubora kwenye kuanzisha mashambulizi.

Kwa kawaida timu inapocheza aina hii ya mpira hutakiwa kuwa na kipa ambaye atakuwa na uwezo mkubwa na kucheza na mpira mguuni ili awe mtu wa kwanza kuanzisha mashambulizi kwa haraka - hii itasababisha timu husika kuwa na faida ya kuikuta timu pinzani ikiwa haipo kwenye umbo lake sawasawa hivyo inakuwa ni rahisi kuifunga. Moja kati ya mifano hai ni kilichotokea kwa kipa wa zamani wa timu ya Taifa ya England, Joe Hart ambaye baada ya Pep Guardiola kupewa mikoba ya kuinoa Man City alimuondoa kikosini kwa kuwa hakuwa na uwezo wa kucheza mpira kwa miguu na badala yake akasajiliwa Claudio Bravo.

 

MABADILIKO YA NIYONZIMA

Juzi Kaze alianza kumtumia Niyonzima kwenye eneo la kiungo cha uchezeshaji, lakini katika kipindi cha pili alimfanyia mabadiliko na nafasi yake ikachukuliwa na Nchimbi lakini majukumu yake alipewa Farid Mussa.

Miongoni mwa wachambuzi wa masuala ya soka Mwalimu Alex Kashasha alisema: “Ukimuangalia Niyonzima ana akili ya mpira na ana uwezo mkubwa wa kupandisha timu na kupiga pasi, lakini hawezi kucheza mpira wa nguvu jambo lililosababisha muda mwingi kuwa anapoteza baadhi ya mipira muhimu.

“Kaze ni kocha mzuri, ukiangalia Yanga unaona mabadiliko, apewe muda afanye kazi yake.”

Kaze mwenyewe aliongeza kuwa: “Bado (Niyonzima) hawajaonyesha kufanya vile ambavyo ninataka kwa asilimia zote, lakini naamini huu ni mwanzo na hapo baadaye wanaweza kuzoea, hatukuweza kutengeneza nafasi nyingi na hata hizo chache hatukuwa na usahihi kwenye kuzitumia.” Anasema alichopenda zaidi kwa wachezaji wake ni hali ya kujituma waliyoonyesha kuanzia kwenye mazoezi na mechi mpaka wakafanikiwa kupata ushindi huo.

“Wachezaji wote wanaweza kucheza,” alisisitiza.