Kahata, Gadiel waikamia kutokea kwa UD Songo

Wednesday August 21 2019

 

By Olipa Assa

Dar es Salaam. Kitendawili cha Simba kusonga mbele Ligi ya Mabingwa Afrika, kitateguliwa Jumapili ya wiki hii katika mechi ya marudiano na UD Songo, itakayopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mastaa wa timu hiyo, wameapa kutoa kichapo kwa UD Songo huku wakiwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia kandanda safi na kuwaahidi hawatawaangusha.

Beki mpya wa timu hiyo, Gadiel Michael amesema wamefanya mazoezi ya kutosha na akili zao zipo tayari kwa ajili ya kupambania timu yao kuhakikisha wanaishushia kichapo UD Songo, kubwa zaidi amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi.

"Ni hamu ya kila mchezaji kuona anapambana kwa kadri anavyoweza ili mladi tu tunashinda mechi ya Jumapili, tuna ari ya mchezo, mashabiki waje kwa wingi kwani uwepo wao ni muhimu kwetu," alisema Gadiel.

Naye Francis Kahata alisema mechi yao ya UD Songo ni nafasi yao ya kipekee kuhakikisha wanaifunga ili kupata chansi cha kusonga mbele kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Alisema wanatambua kazi walionayo kuwa ngumu, akisisitiza ndio wakati wao wa kujitoa kwa kadri watakavyoweza ili kuhakikisha wanashinda mchezo huo.

Advertisement

"Hakuna kazi rahisi kitu chochote chenye mashindano ujue kuna wakushinda na kushindwa, tumejipanga kuhakikisha tunapata ushindi kubwa zaidi tunahitaji kufika mbele kwenye michuano hiyo," alisema Kahata.

Advertisement