Kagere, Dube wajiangalie

UKIACHANA na wachezaji Meddie Kagere (Simba) na Prince Dube wa Azam FC, nyota wa Gwambina FC, Meshack Abraham naye ameonekana kuja kwa kasi katika Ligi Kuu kutokana na kuwatesa makipa.

Hadi sasa Dube anayekipiga Azam FC ndiye kinara wa mabao kutokana na kufunga mabao sita baada ya mechi sita, huku Kagere akifuatia kwa mabao manne mechi tano.

Hata hivyo Abraham ambaye ni msimu wake wa kwanza Ligi Kuu juzi akiisaidia timu yake ya Gwambina kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar aliweza kutupia bao lake la tatu msimu huu.

Mbali na idadi hiyo kwa kinda huyo, lakini pia aliweka rekodi ya kufunga katika mechi mbili mfululizo akianza dhidi ya Ihefu alipofunga mabao mawili ambayo yaliipa alama tatu timu yake.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Novatus Fulgence alisema licha ya kwamba nyota huyo hatajwi, lakini amekuwa moja ya wachezaji kikosini wenye faida katika mafanikio hadi sasa.

Alisema kutokana na kasi aliyoanza nayo huenda huko mbeleni akafanya makubwa zaidi kwani uwezo na ubunifu alionao uwanjani anaweza kushindana na maproo wa timu yoyote.

“Hapa wanatajwa wachezaji wa timu nyingine wanamsahau huyu Abraham, lakini ni mchezaji mwenye uwezo na amesaidia sana hadi sasa mafanikio ya Gwambina tulipo na tunategemea makubwa zaidi huko mbeleni,” alisema Fulgence. Kutokana na mabao matatu aliyofunga nyota huyo katika mechi mbili mfululizo yameifanya Gwambina kuchumpa hadi nafasi ya nane kwa pointi saba baada ya mechi sita.