KMC yaliamsha dude mapema

Friday August 23 2019

 

By Yohana Challe na Olipa Assa

KAMA kuna jambo ambalo AS Kigali ya Rwanda haitaki kulisikia ni mpango uliotengenezwa na Kocha Jackson Mayanga katika mechi ya leo, akitaka vijana wake wamelize kazi mapema ili wasonge mbele katika michuano ya Kombe la Shirikisho.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa wiki mbili zilizopita Kigali, KMC iliwabana vilivyo wenyeji wao na kutoka suluhu, lakini Mayanja amewataka jamaa hao wasahau sare mbele yao kwani mipango yake ni ushindi ili watinge raundi ya kwanza.

“Tupo tayari kwa vita hii, nimejitahidi kuwajenga wachezaji wangu na kiu kubwa ni kuona tunashinda, tunajua sare yoyote ni hasara kwetu, ndio maana tunataka ushindi,” alisema.

Alisema atawatumia viungo wengi katika kuhakikisha wanapata ushindi kwani safu yao ya ushambuliaji itawakosa baadhi ya nyota wao walio majeruhi.

“Nitafanya kila linalowezekana ili kushinda mchezo huo hapa nyumbani na hicho ndicho ninachokiamini, hakuna nafasi nyingine tunayoweza kuitazama ili kutuvusha,” alisema.

Hata hivyo, jambo zuri ni kurejea tena kwa James Msuva na Salim Aiyee na Charles Illafya waliokuwa majeruhi, japo itawakosa washambuliaji wengine watatu.

Advertisement

Daktari wa timu hiyo, Dk Sebastian Mapunda alisema Ramadhani Kapela aliyeumia mguu wa kulia kwenye michuano ya Kombe la Kagame hatacheza dhidi ya AS Kigali na ataanza kuonekana uwanjani wiki ijayo.

Dk Mapunda alisema Cliff Buyoya aliyeumia goti na atafanyiwa upasuaji, huku Serge Nogues aliyeumia kifundo cha mguu atakaa nje kwa wiki mbili.

Advertisement