KARIBUNI MACHINJIONI: Watakaoanza Yanga, Simba ni hawa

Tuesday June 2 2020

 

By WAANDISHI WETU

SIO siri hakuna siku ambayo klabu za mikoani zilikuwa na raha kama jana. Tamko la serikali kuwa, Ligi sasa zitapigwa nyumbani na ugenini liliwafurahisha kwelikweli huku wakisisitiza kwamba sasa ni wakati wa wakubwa kuja machinjioni. Wakimaanisha ugenini.

Awali kulikuwa na mvutano baina ya wadau mbalimbali wa soka wakipinga taarifa za Wizara kupendekeza mechi zipigwe katika vituo.

Waziri wa Habari Utadmaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alikakariwa akisema Ligi Kuu Bara na Kombe la FA zitachezwa Dar es Salaam huku Daraja la Kwanza na La Pili zingekuwa Mwanza.

Yanga, Simba na Azam zilionekana kufurahishwa zaidi na uamuzi wa kituo kimoja kutokana na rekodi zao haswa wanapokuwa viwanja bora za Dar es Salaam.

Habari za ndani kutoka katika Bodi ya Ligi ni kwamba katika ratiba ambayo itatoka leo Saa 4 asubuhi, Yanga na Simba wataanza na viporo vya kwanza ili waende sawa na wenzao. Ambapo Yanga ana viporo vya Mwadui, Azam na JKT huku Simba akiwa na Ruvu Shooting na Mwadui.

Serikali imefikia uamuzi wa jana, baada ya kujadiliana na wadau mbalimbali wa soka nchini ili kuwa na namna nzuri ya kumalizia michezo hiyo iliyobaki katika kipindi hiki ambapo pia maambukizi ya corona yamepungua.

Advertisement

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Hassan Abbas ilisema Ligi Kuu Bara na shughuli zote za kimichezo zitaendelea kuanzia leo kwa kuzingatia mwongozo wa Afya michezoni.

“Serikali kupitia wizara yenye dhamana na Afya ilishatoa mwongozo wa Mei 28,2020, unaoelezea hatua za kuchukua katika kila hatua za kuendesha michezo nchini,” alisema Abbas na kuongeza;

“Mwongozo huo ni pamoja na Elimu kwa wadau wa michezo kuhusu kujikinga na maambukizi, Kambi viwanja vya mazoezi na Mechi kuwezesha upatikanaji wa maji tiririka na sabuni kwa akili ya kunawia mikono au vipukusa (Sanitizers).

“Usalama wa wachezaji na viongozi, Mazingira mengine wakati wa mazoezi na mashindano hapo mashabiki hawataruhusiwa kusababishwa misongamano na vifaa vya michezo vitatakiwa kusafishwa.”

Kuhusu mashabiki alisema; “Wataruhusiwa kwa utaratibu wa kawaida isipokuwa katika mechi zitakazoonekana zinaweza kujaza uwanja hapo kanuni ya kuruhusiwa mashabiki wasiozidi nusu ya uwanja itumike, ili kila mmoja akae umbali wa mita moja kama inavyotakiwa.”

Upande wake Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wallace Karia aliishukuru Serikali na kuahidi kwa nafasi yao kama shirikisho watahakikisha kila jambo linaenda sawa.

Pia alisema klabu wataendelea kupata mikwanja yao kama kawaida kupitia viingilio ambapo mwenyeji atachukua asilimia 60 ya mapato.

KLABU SHANGWE TUPU

Kauli ya serikali imepokewa kwa shangwe na klabu zilizoshangilia kwelikweli.

“Ni taarifa ambayo imekuwa na busara zaidi kwa klabu, kucheza nyumbani na ugenini itasaidia kupunguza gharama kwaajili ya kambi na kukodishwa viwanja kama kituo kimoja kingetumika kwaajili ya michezo iliyosalia,’ alisema Katibu Mkuu wa Tanzania Prisons, Ajabu Kifukwe.

Naye Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime alisema maamuzi yoyote kwake sawa tu, kwa vile watoa maamuzi ndio wasimamizi wa mpira na wao ni watekelezaji tu.

Alisema, hata awali waliposema mechi zitachezwa Dar es Salaam pekee, timu yake ilikuwa tayari kwa mapambano katika sehemu yoyote ile.

Kwa upande wa Alliance kupitia kwa Kocha Mkuu, Kessy Mziray alisema; “Nasema kwa dhati kabisa, serikali imechukua maamuzi sahihi, kwanza kanuni ilikuwa inabana na kubadilisha kanuni sio jambo la kawaida, hivyo ni vyema tumalize kama kanuni zinavyosema.”

“Kikubwa wachezaji na mashabiki wanatakiwa kuwa makini na kujikinga dhidhi ya maambukizi ya kuenea zaidi kwa ugonjwa wa covid 19,” aliongeza

Makamu Mwenyekiti wa Polisi Tanzania, Robert Munis alisema, wao walikuwa tayari kwa mapambano ya aina yoyote ambayo serikali kwa kushirikiana na TFF ingeyaamua.

Katibu wa KMC, Walter Harrison alisema wengi walipenda kuona ligi inaendelea na bingwa apatikane uwanjani, kuhusu maamuzi ya kuchezwa kama awali pia ni maamuzi sahihi na ndio faraja kwa timu nyingi.

Naye Mwenyekiti wa Biashara United, Seleman Mateso alisema hatua hiyo itawaweka huru Shirikisho la Soka nchi ,(TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB) kwa timu itakayoshuka kwani hakutakuwa na visingizio.

“Huu ndio uongozi tunaoupenda niwashukuru na kuwapongeza serikali kwa maamuzi haya, hapa kazi ni kwetu kupambana, TFF na Bodi ya Ligi wamejivua msala huko mbeleni, malalamiko hayatakuwapo,” alisema Mateso.

Katibu Mkuu wa Kagera Sugar, Ally Masoud alisema; “Hapa nasi Kagera Sugar huenda tukafikia malengo yetu ya kuwania nafasi zile tatu au nne za juu.”

Naye Kocha Mkuu wa Mwadui FC, Khalid Adam alisema hatua hiyo wameipokea kwa shangwe kwani mbali na matokeo nyumbani lakini inasaidia kupunguza hata gharama za kambi nje na mengineyo.

“Mtu anapokuwa nyumbani anakuwa na faida kubwa hata matokeo kwa sababu timu nyingi unakuta zimezoea uwanja wake kwahiyo maamuzi haya sisi tumeyapenda sana,” alisema Adam.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda alisema licha ya maamuzi hayo mazuri, lakini TFF na Bodi ya Ligi wanapaswa kuwa makini haswa kwa dakika hizi wakielekea mwishoni.

Alisema Ligi ilianza vizuri na hadi sasa hakuna tatizo, lakini kwa timu haswa zinapombana kuwania nafasi zile za juu na kutoshuka Daraja, inaweza kutokea figisu hivyo lazima umakini na ufuatiliaji uwepo ili kudhibiti hali hiyo.

“Ni sawa maamuzi ni mazuri na Ligi yetu inaendelea vyema hadi sasa, lakini nishauri TFF na Bodi ya Ligi wawe makini haswa hizi mechi za mwisho kuondoa sintofahamu kwa timu zinazowania nafasi fulani” alisema Mgunda.

IMEANDIKWA NA ELIYA SOLOMON, YOHANA CHALLE, SADDAM SADICK NA CLEZENCIA TRYPHONE

Advertisement