Juve wabeba tena ndoo ya Serie A

Muktasari:

Huo unakuwa ni ubingwa wa wa tisa mfululizo kwa Juve, huku ikiwa imemaliza msimu kwa jumla ya alama 83, nyuma ya Inter Milan yenye alama 82.

Turin, Italia. LIGI Kuu Italia (Serie A) inamalizika usiku wa leo Jumapili, lakini jana kulipigwa mechi kadhaa huku ikishuhudiwa kwa mara ya tisa mfululizo 'Kibibi cgha Turin', Juventus wakibeba tena ubingwa, licha ya kupoteza nyumbani dhidi ya AS Roma kwa kupigwa mabao 3-1.

Juve imemaliza msimu kwa kukusanya pointi 83, moja zaidi ya wapinzani wao Inter Milan ambao msimu huu walikuwa moto kwelikweli na waliomaliza na ushindi ugenini wa 2-0 na kufikisha alama 82.

Katika mchezo wa Inter dhidi ya Atalanta waliomaliza nafasi ya tatu na alama zao 78, timu zote zilionyesha ushindani wa hali ya juu, lakini ni Inter waliotoka na ushindi huo na kuwaacha wenyeji wao wakilingana na Lazio ambao nao wamemaliza kwa kichapo cha 3-1 ugenini dhidi ya Napoli na kuwafanya wenyeji kumaliza nafasi ya saba na alama zao 62.

AC Milan nayo ikiwa  nyumbani ilitakata kwa kuinyoa Cagliari na kumaliza nafasi ya sita ikiwa na pointi 66 na kukata tiketi ya kucheza Europe League msimu ujao.

Mchezo wa mwisho ulikuwa kati ya Brescia ambayo tayari imekata tiketi ya kushuka daraja ilipoumana  dhidi ya Sampdoria, mchezo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, Sampdoria imemaliza ikiwa nafasi ya 15 ikiwa na alama 42.

Ligi hiyo itaendelea usiku wa leo kwa mechi nyingine tano kwenye uwanja wa Paolo Mazza, SPAL itakuwa na shughuli mbele ya Fiorentina mchezo utapigwa saa 1:00 usiku, Bologna itaumana na Torino saa 3:45 usiku. Sassuolo iliyopo nafasi ya nane na alama zake 51, itakipiga dhidi ya Udinesse iliyopo nafasi ya 14, ikiwa na alama 42 mchezo utapigwa saa 3:45.

Genoa inayoshika nafasi ya 17 itakuwa mwenyeji wa huku Hellas Verona iliyopo nafasi ya tisa na alama zake 49 mchezo utapigwa saa 3:45 usiku, pale katika dimba la Stadio Comunale Via del Mare wenyeji Lecce watailika Parma katika mchezo ambao pia utapigwa saa 3:45 jioni.