Julio ampaisha Jabir

Muktasari:

Kocha Jamhuri Kihwelu 'Julio' ni kama ameipa wepesi ndoto ya mshambuliaji wa Dodoma Jiji, Anual Jabir, ambaye anataka kucheza soka nje, hii ni baada ya kumuita Ngorongoro Heroes.

 

KITENDO cha kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 20 'Ngorongoro Heroes', Jamhuri Kihwelu 'Julio' kumuita kwenye kikosi chake straika wa  Dodoma Jiji, Anual Jabir ni kama kumetimiza ndoto za mchezaji huyo.

Jana Ijumaa ya Oktoba 23, mwaka 2020 kocha Julio alitangaza kikosi hicho, kitakachojiandaa na michuano ya Cecafa itakayoanza Novemba 10 hadi Desemba 20, Tanzania ikiwa mwenyeji na imepangwa kufanyika mkoani Arusha.

Jabir ameliambia Mwanaspoti online, leo Jumamisi ya Oktoba 24, mwaka 2020 kwamba ilikuwa ndoto yake kucheza ligi kwa mara ya kwanza msimu huu, aonekane na kuitwa timu ya taifa.

Jabiri alianza kutikisa Ligi Daraja la Kwanza, akiwa na Dodoma Jiji na baada ya kupanda amekuwa akifanya vizuri, amesema kocha Julio kumuita kwenye kikosi cha Ngorongoro Heroes, kunamuongezea mwendo wa kuelekea ndoto zake za kucheza nje.

"Nimefurahi kocha kunijumuisha kwenye kikosi chake, kwani ni muda mwafaka wa kuonyesha kipaji changu ndani na nje ya nchi, jambo linaloweza kunifungulia njia ya kufika mbali,"amesema Jabir na ameongeza kuwa,

"Hii ni fursa kubwa kwangu kujituma kwa bidii, kuhakikisha nafikia malengo yangu kwasababu nimechagua soka kuwa sehemu ya kunipatia kipato, kitakachokuwa kinasaidia kuendesha maisha yangu,"amesema.