JKT yaichapa Oilers nusu fainali RBA

Muktasari:

Mpaka sasa JKT ndiyo timu pekee ambayo haijafungwa kwenye RBA, imecheza mechi 18, 15 zikiwa za Ligi na mbili za robo fainali 'playoff' na kushinda zote

 OILERS imeanza kwa kipigo katika mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Ligi ya mpira wa kikapu mkoa wa Dar es Salaam (RBA) jana Alhamisi usiku.

Timu hiyo iliangukia 'pua' mbele ya maafande wa JKT kwa kuruhusu kipigo cha pointi 59-46 kwenye Uwanja wa Bandari, Kurasini.

 Katika mechi hiyo iliyokuwa ya ushindani, JKT ilichomoza na ushindi wa kwanza kwa tofauti ya pointi 13.

 Kwa matokeo hayo, JKT itahitaji kushinda mechi nyingine mbili ili kufuzu kucheza fainali ya RBA, vinginevyo timu hizo zitalazimika kucheza mechi tano.

 Mshindi wa mechi tatu ndiye atafuzu kucheza fainali na mshindi wa mechi kati ya ABC na Kurasini Heat, ambao wataanza kusaka tiketi ya fainali leo ijumaa usiku uwanjani hapo.

 Mbali na matokeo hayo, vita ya ufungaji hivi sasa imehamia kwa nyota wa JKT, Baraka Sadiki, Enrico Augustino wa ABC na Herve Mbaya  wa Oilers.

 Enrico ndiye anaongoza mpaka sasa akiwa amefunga pointi 365, ame-assist mara 44 na kuchukua mipira inayorudi mara 51, akifuatiwa na Baraka ambaye amefunga pointi 350, ame-assist mara 37 na kuchukua rebounds mara 39.

 Jonas Mushi anawafuatia akiwa na pointi 327 ingawa timu yake ya Vijana tayari imeondoshwa mashindanoni na Herve ni wanne kwenye msimamo wa wafungaji akiwa na pointi 301, ame-assist mara 34 na kuchukua rebounds mara 72.