JAMVI LA KISPOTI : Amunike ataondoka, atatuachia matatizo yetu

Muktasari:

  • Tangu ameanza kazi amefanikiwa kupata mechi mbili tu za mazoezi dhidi ya Misri na ile ya Zimbabwe tena wakicheza siku chache kabla ya kuanza kwa fainali za Afcon.

TANZANIA nayo imemtimua kocha wao Emmanuel Amunike’, sentesi moja anaandika rafiki yangu mwandishi wa habari kutokea Misri, Fareed Kotb baada ya hapo akaweka vikatuni vikionyesha anacheka kwa uamuzi huo kufuatia taarifa hiyo, nami ikanibidi nicheke sasa nifanye nini!

Unajua kwanini Kotb anacheka? Aliiona Taifa Stars kule Misri kisha akashangazwa kuona timu yetu ikiwa na wachezaji wa kawaida halafu tukiwa tumefuzu Fainali za Mataifa Afrika hali ya kuwa hakukuwa na nafasi ya mshindwa bora (best loser).

Sikushangazwa sana na uamuzi huo lakini nilichokuja kugundua ni kwamba uamuzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumfuta kazi Amunike ni kama kumuondoa kocha huyo ili sisi tubaki na matatizo yetu.

Ukweli ni kwamba Amunike ataondoka, lakini kuondoka kwake hakutufanyi kumaliza matatizo yetu ya ndani ambayo yako mengi kuliko yale ya Amunike.

Unamuondoaje Amunike wakati umemleta awe kocha wa timu yako kisha ukashindwa hata kumtafutia mechi za kirafiki halafu ukataka mafanikio afanye vizuri?

Tangu ameanza kazi amefanikiwa kupata mechi mbili tu za mazoezi dhidi ya Misri na ile ya Zimbabwe tena wakicheza siku chache kabla ya kuanza kwa fainali za Afcon.

Unatinga Afcon halafu unamtimua Mkurugenzi wa Ufundi ambaye ndiye mtu anayetakiwa kufanya kazi kwa karibu na Amunike katika kufanya uimara wa kazi zake za kila siku.

Mpaka tunatakiwa kujiandaa na fainali za Afcon hatukuwa na Mkurugenzi wa Ufundi ambaye kama Amunike angehitaji kitu angekuwa anaelewa lugha ambayo kocha huyo anasema nini kutokana na wote wanajua kile kinachohitajika.

Shida yetu kubwa tuna viongozi ambao nao ni makocha, wanajua kila kitu na ndiyo maana Amunike alipohitaji vifaa vya mazoezi havikununuliwa, lakini waliposema jambo hilo hilo wataalam wa kule Misri ambao waliongeza nguvu, vikanunuliwa haraka.

Tunamtimua Amunike hali ya kuwa si yeye aliyetusababishia wachezaji wetu baadhi kukosa msingi bora wa maandalizi tangu wakiwa wadogo na hata baadhi kukosa nidhamu.

Tuna wachezaji ambao wanaitwa kambini kujiunga na timu ya taifa wiki mbili kabla, lakini wakaja kujiunga siku moja kabla ya timu kwenda Misri halafu tunatarajia kupata mafanikio.

Tuna wachezaji ambao wanashindwa hata kutuliza mpira na kutoa pasi na kumfanya kocha kuwa na kazi kubwa ya kuanza kufundisha watu wazima kana kwamba anafundisha timu ya watoto wa miaka 10.

Tuna ligi dhaifu inayoshindwa kuzalisha mchezaji sahihi inayoendeshwa kwa maelekezo ya simu za mkononi na fitna halafu tunajiangalia na kujiona tunajua na kwamba Amunike anatupotezea muda.

Ligi yetu haina ubora wa kutoa mchezaji wa kucheza Afcon halafu akatupa matokeo yaliyo bora kama ambavyo tulijiandaa kupata ushindi.

Nchi yetu bado tuna viongozi ambao bado wanahitaji kwenda katika vyumba vya wachezaji mpaka sasa kutoa maelekezo wakati wa mapumziko, tunaishi dunia ya pekee yetu sana.

Nionavyo mimi bado tuna matatizo makubwa kuliko Amunike na maamuzi ya kumuondoa kocha ni kama tunataka kujificha katika kivuli chake.

Kansa katika mpira wetu ni kubwa, bahati mbaya daktari aliyekuwa akijaribu kutuongezea siku za kuishi tukamuondoa, kinachofuata hapo ni nini kama siyo kifo?

Tulijimaliza katika kukubaliana na baadhi ya watu kuingia katika mpira wetu ambao wanataka kuishi kirafiki na sio kwa weledi hatua ambayo sasa inatumaliza.

Kabla ya kumfuta kazi Amunike je tulijiuliza mambo ya msingi?

Tulimpa malengo gani wakati akisaini mkataba wa kuifundisha Stars?

Katika malengo tuliyompa alifaulu kwa kiasi gani na alishindwa kwa asilimia ngapi?

Kama yalikuwapo malengo tuliyompa na mojawapo likawa ni kuiwezesha Stars kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 39. Basi hilo alifaulu.

Swali jingine, linafuata. Baada ya lengo hilo, tulimpa lengo la kuvuka hatua ya makundi na kutinga hatuia ya 16-Bora.

Kama tulimpa lengo hilo basi alishindwa.

Lakini ni kweli kwamba Watanzania tulitarajia kuwafunga Algeria na Senegal kule Misri?

Nenda Amunike kapumzike, karibu tena kutembelea mbuga zetu na kiwanja chako ulichopewa na Rais John Magufuli kule Dodoma kama utaamua kujenga sawa unaruhusiwa, lakini tuachie matatizo yetu, maana haya tumeyapenda zaidi kuliko utaalam wako.