Ishu ya ubaguzi Eymael moto unawaka

Muktasari:

Makamu mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema wao kama klabu hawaungi mkono masuala ya kibaguzi, lakini TFF imekosea kutoa waraka kumshutumu na kumlaumu aliyebaguliwa.

WAKATI uamuzi wa sakata la kocha wa Yanga, Luc Eymael na mwamuzi Hans Mabena ukisubiriwa kutoka Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Kamati ya Saa 72), Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Chama ameifungukia ishu hiyo.

Baada ya mchezo kati ya Yanga na Azam uliofanyika Jumamosi iliyopita, Eymael alikaririwa akimlalamikia Mabena kwa kukataa mkono wake baada ya mchezo huo kumalizika, hivyo kukiita kitendo hicho kuwa ni kama ubaguzi dhidi yake.

TFF ilitoa taarifa kuwa kauli za ubaguzi wa rangi hazina nafasi kwenye soka la Tanzania kwani kama nchi haina historia na haiungi mkono vitendo hivyo au ajenda zinazochochea ubaguzi wa rangi, hivyo matarajio yao Kamati ya Saa 72 italifanyia kazi suala hilo lililojitokeza katika mchezo huo na kuchukua hatua kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu.

“Hilo sakata kwa sababu limepelekwa Kamati ya Saa 72 acha tusubiri uamuzi wake,” alisema Chama.

Aliongeza: “Ila kwa jinsi yule kocha alivyokuwa anambughudhi mwamuzi hata ningekuwa mimi nisingempa mkono. Alijenga dhana kwamba anaonewa, hivyo tayari walishajenga chuki baina yao na yule mwamuzi ana nyongo na kama unavyojua mtu yeyote mwenye nyongo anakuwa na hasira.

“Pia ukiangalia kwa undani zaidi, kitendo cha kocha kumpa mkono mwamuzi ilikuwa kama kejeli kwani awali mwamuzi alimuonyesha kocha kadi ya njano, hivyo kitendo cha kutaka kumpa mkono baada ya mechi alichukulia kama anamkejeli.”

Mchambuzi wa soka, Ally Mayay alisema: “Tatizo kubwa hapo ni tafsiri ila kwa tukio la masuala ya kibaguzi wala sidhani kama ni sahihi kwani tamaduni za soka letu hatujawahi kuwa na matukio kama hayo.

“Matukio ya watu kutopeana mikono yameshatokea mara kwa mara, ila kwa sababu ya ugeni wa kocha wa Yanga ukasababisha kuhisi labda inawezekana kwa sababu yeye ni rangi nyingine, labda ndio maana hakupewa mkono, hivyo ni tafsiri yake tu lakini wala halina uhusiano wowote na ubaguzi.”

Makamu mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema wao kama klabu hawaungi mkono masuala ya kibaguzi, lakini TFF imekosea kutoa waraka kumshutumu na kumlaumu aliyebaguliwa.

“Matumaini yetu makubwa TFF itamchukulia hatua kali mwamuzi aliyekataa kupewa mkono na kocha wetu ambaye alikuwa akionyesha mchezo wa kiungwana,” alisema Mwakalebela.