Hawashikiki wanapovaa uzi wa timu za Taifa

Muktasari:

  • Hawa hapa mastaa ambao wanacheza vizuri zaidi wakiwa na timu za taifa kuliko kwenye klabu zao.

LONDON,ENGLAND. KUNA mastaa kibao wamekuwa wakichemsha kwenye soka la kimataifa, wakishindwa kucheza kwa viwango vya juu kama wanavyofanya kwenye klabu zao.

Mmoja kati ya mastaa hao ni supastaa Lionel Messi, ambaye siku zote kiwango chake anapokuwa kwenye kikosi cha Argentina ni tofauti kabisa na anavyokuwa na uzi wa Barcelona.

Lakini kuna wachezaji hao wamekuwa kinyume chake, wanapokuwa na jezi za timu za taifa wanakuwa watamu kinoma, tofauti wanapozichezea klabu zao.

Hawa hapa mastaa ambao wanacheza vizuri zaidi wakiwa na timu za taifa kuliko kwenye klabu zao.

5. Asamoah Gyan(Ghana)

Asamoah Gyan, aliwashangaza wengi baada ya kuamua kusitisha uamuzi wake wa kustaafu soka na kuamua kurudi kuitumikia Timu ya Taifa ya Ghana baada ya kuzungumza na rais wa nchi hiyo kwa ajili ya michuano ya Afcon 2019.

Kilikuwa kitu kisichoshangaza kuona amepokewa kwa mikono miwili kutokana na ubora wake anapoitumikia timu ya Ghana kwenye soka la kimataifa, akiweka rekodi ya kuwa kinara wa mabao wa muda wote, akifunga mara 51 katika mechi 106.

Kwenye soka la klabu, Gyan anakuwa mtu tofauti sana, anashindwa kucheza kwa kiwango bora na ndio maana amekuwa mtu wa kuhama mara Ufaransa, Italia, England, China, Uturuki na siku za karibuni amekuwa huko Falme za Kiarabu.

4. Keisuke Honda(Japan)

Keisuke Honda bila ya utata wowote amekuwa mmoja kati ya wanasoka mahiri kabisa katika historia ya Japan, tangu alipoibukia kwenye michuano mikubwa akifunga mara mbili na kuasisti katika fainali za Kombe la Dunia 2010.

Kiungo huyo mshambuliaji amekuwa mchezaji wa kwanza wa Japan kufunga mabao katika fainali tatu mfululuzo za Kombe la Dunia akiwa na jezi za Japan. Lakini mambo yake yamekuwa tofauti kabisa anapokuwa kwenye soka la ngazi ya klabu, amekuwa hana makali kabisa ya kutisha licha ya kubahatika kucheza kwenye timu kubwa Ulaya kama AC Milan. Alipotoka hapo, alirudi kwao Japan na sasa amekuwa akifanya tu shughuli za ukocha kwenye Timu ya Taifa ya Cambodia.

3. Xherdan Shaqiri (Uswisi)

Licha ya kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Bayern Munich na baadaye akiwa na Liverpool, Xherdan Shaqiri bado hajacheza kwa kiwango kikubwa sana kwenye soka la klabu ukilinganisha na anavyokuwa kwenye majukumu ya kuitumikia timu yake ya taifa ya Uswisi.

Winga huyo ameifungia timu yake ya taifa mabao 22, huku baadhi ya mabao hayo yakiwa kwenye mechi muhimu za michuano mikubwa iliyoshiriki timu hiyo. Waswisi huwaambii kitu kuhusu Shaqiri.

2. James Rodriguez (Colombia)

Mshindi wa Kiatu cha Dhahabu kwenye fainali za Kombe la Dunia 2014 zilizofanyika Brazil. Staa James Rodriguez aliweka jina lake juu kwenye anga za soka baada ya kufanya kwenye fainali hizo akiwa na kikosi cha Colombia Kombe la Dunia 2014.

JLakini utashangaa staa huyo amekuwa akishindwa kuonyesha makali katika timu yake ya klabu, ambapo amechemsha huko Real Madrid na kujikuta akitolewa kwa mkopo Bayern Munich, ambako pia haina mpango wa kumpa dili la moja kwa moja baada ya mkopo wake wa misimu miwili.

1. Alexis Sanchez (Chile)

Kama kuna mchezaji ambaye Manchester United inaweza kushawishika kumtoa bure basi ni Alexis Sanchez kutokana kiwango chake cha soka anachokionyesha kwenye kikosi hicho. Man United haijafurahia kitu kutoka kwa staa huyo tangu ilipomsajili kutoka Arsenal Januari mwaka jana huku ikimlipa mshahara mkubwa sana kwa wiki. Lakini anapokuwa na jezi za Timu ya Taifa ya Chile, Sanchez anakuwa tofauti sana na ameshafunga mabao 43 ya Chile.