Harun Shakava: Mkali aliyetemwa harambee Stars, awazia makubwa

Wednesday June 5 2019

 

By Thomas Matiko

BAADA ya kutemwa kwenye kikosi cha taifa, Harambee Stars kilichokwenda Paris, Ufaransa kwa ajili ya kambi ya mazoezi ya wiki tatu kujiweka sawa kwa michuano ya AFCON 2019, nahodha wa Gor Mahia, Harun Shakava aliumia sana.

AKAWAZIA KUSTAAFU

Shakava ambaye amekuwa kwenye kikosi cha Stars kwa miaka kadhaa kabla ya ujio wa Kocha Mfaransa Sebastian Migne, anasema baada ya kutemwa na mzungu huyo, ilimuuma sana kiasi aliwazia kustaafu soka la kimataifa.

Katika fikra zake, haikumtokea ipo siku angetemwa kwenye kikosi cha taifa kutokana na mchango wake kwa klabu yake hasa baada ya kuisaidia kubeba ubingwa wa Ligi Kuu mara tatu mfululizo. Msimu huu aliwaongoza tena wenzake kutwaa taji lao la 16.

Kilichomuumiza hata zaidi Shakava ni pale Kocha Migne aliamua kumwacha pia nje ya kikosi atakachokitumia kwenye dimba la CHAN litakalofuata baada ya AFCON.

“Awali niliwazia kustaafu kiuichezea timu ya taifa ila baada ya kutakafari kwa kina na kwa ushauri wa baadhi ya watu wangu wa karibu nilighairi,” Shakava anasema.

Advertisement

Aidha kilichombadilisha mawazo hata zaidi ni pale alipoona sio yeye tu aliyetemwa kikosini, bali pia straika matata anayesumbua kule Zambia, Jesse Were aliyezua gumzo sana baada ya Kocha Migne kumwacha licha yake kuwa katika fomu nzuri.

“Kikweli ilinishtua sana kocha aliponiacha, pia alimwacha Jesse Were hapo nikatulia kidogo. Isitoshe haya hutokea kote duniani lakini hata zaidi bado mimi ni mchanga na nitaendelea kupambania nafasi yangu,” Shakava akazidi.

TETESI ZA BIFU KATI YAKE NA MIGNE

Baadhi ya tetesi nyanjani zinadai uamuzi wa Kocha Migne kumwacha nje Shakava ilikuwa ni adhabu kwa beki huyo kwa kumyeyushia mwaka jana.

Migne alimwita Shakava kwenye kikosi alichosafiri nacho mwaka jana kushiriki dimba la Hero Continental Cup kule India.

Hata hivyo, Shakava alilenga mwito huo na badala yake akasafiri na Gor kwenda kushiriki dimba la Cecafa kagame Cup. Ni taarifa ambazo anaonyesha kuziamini ila Shakava anakuwa makini kukwepa kujiweka kwenye mashaka zaidi.

Huku akimtema kwenye kikosi, Migne aliwajumulisha mabeki wawili wenzake kutoka Gor, Joash Oyango na Charles Omanyi.

Shakava anajitia hamnazo kutoelewa ni kwa nini wenzake walijumulishwa huku akiachwa yeye wakati akisisitiza yupo vizuri zaidi ya wenzake.

“Kwenye difensi mimi naongoza kwa ubora ukizingatia muda wa mchezo hivyo sielewi kilichotokea wenzangu wawili ninaowapiku kwa takwimu hizi walichukulia nikaachwa mimi. Hata hivyo, lililokolezwa ishu ya ikiwa kutemwa kwake ni adhabu ya kumchorea giza Kocha Migne alipomhitaji mwaka jana, Shakava aligeuka mwanafilosofia.

“Sidhani kama kuachwa kwangu ni suala la siasa au nidhamu kama ninavyosikia. Sababu  kama  ndivyo ilivyo bas naye Jesse Were asingeachwa pamoja na wachezaji wengine kibao wazuri tu waliotemwa.”

AZUNGUMZIA MAISHA GOR NA UBINGWA

Beki huyo wa miaka mingi pale Gor, anasisitiza kuwa ubingwa wao wa mara tatu mfululizo umetokana na wao kujituma na kudumisha nidhamu uwanjani.

Toka alipojiunga na Gor, Shakava ameishia kutwaa ubingwa mara tano huku tatu za mwisho akiwa kama nahodha.

Shakava alijiunga na Gor 2014 akitokea Kakamega Homeboyz mwaka mmoja tu baada ya kumaliza masomo yake ya kidato.

Katika miaka yote hiyo mitano aliyokuwa na Gor, kakosa kubeba ubingwa mara moja pekee 2016 Tusker walipopita nalo huku Kogalo wakimaliza  katika nafasi ya pili.

DATA ZAKE

Baada ya kutisha sana na Kakamega Homeboyz iliyomsajili akiwa bado kidato, Gor ilimchukua 2014 baada ya kumaliza na kumpa mkataba wake wa kwanza.

Kipindi hicho akisaini mkataba wake wa kwanza na Gor, Shakava alikuwa na miaka 18 pekee na haikuwa rahisi kwake kupata namba lakini alipambana.

Miaka minne baadaye aliteuliwa nahodha wa Gor akichukua unahodha kutioka kwa beki wa kati aliyekuwa patna wake Musa Mohammed baada yake kuondoka. Hadi kufikia mwisho wa msimu huu, Shakava kaichezea Gor jumla ya mechi 330 huku akiipachikia jumla ya mabao 24 nyingi zikitokana na kichwa.

“Ni furaha kwangu kutwaa ubingwa mara tano na Gor.

Nilipojiunga tulikuwa wachezaji wengi chipukizi ila wengi walishindwa kuendelea sababu ya utovu wa nidhamu. Nilivumilia na kuwa  mwenye subra na mwishowe jitihada hizo zimelipwa,” Shakava alizidin kufunguka.

HATMA YAKE NA GOR

Shakava anaamini kuwa huu ni wakati mwafaka kwake kuondoka Gor huku nyota yake ikiwa inang’aa ili kujaribu taaaluma yake kwingine.

Uongozi wa Gor bado haujamwasilisha mkataba mpya na tayari zipo tetesi kuwa huenda akagur.

“Mkataba wangu unamalizika Desemba mwaka huu nab ado sijawasilishiwa mwingine. Kama wakiniletea nitaitathmini kisha nifanyeb maamuzi. Vile vile zipo ofa kibao nimepokea kutoka Ukanda huu wa Afrika Mashariki, Barani na Ulaya ila bado sijafanya maamuzi.”

Advertisement