Hao kina Sarpong wanakwamia hapa

BAADA ya jumla mechi 36 kupigwa katika Ligi Kuu Bara tangu ianze Septemba 6 na mabao 54 kufungwa (wastani ambao ni mdogo kulinganisha na msimu uliopita), makocha wamefichua kilichosababisha upungufu huo.

Ligi ikiwa ipo raundi ya nne, timu 18 zinazoshiriki zikiwamo zilizosajili nyota waliopewa nafasi kubwa ya kutesa msimu huu akiwamo Michael Sarpong, Waziri Junior, Peter Mapunda na wengine wameonekana hawajakifanya kile kilihotarajiwa kwa kuzalisha mabao machache tofauti na msimu uliopita.

Msimu uliopita, ligi ikishirikisha timu 20, hadi kufikia raundi ya nne kama sasa kulikuwa na mabao 76 yaliyofungwa katika mechi 40 zilizochezwa ikiwa ni wastani wa bao 1.9 kila mechi.

Msimu huu, mabao 54 yaliyofungwa katika mechi 36 za timu 18 ni sawa na wastani wa bao 1.5 kila mechi.

Licha ya timu nyingi kusajili wachezaji wapya hasa katika nafasi za ushambuliaji, lakini wameshindwa kuonyesha cheche na kujikuta timu zao zikifunga mabao machache.

Hata hivyo, inadaiwa kitendo cha makocha wengi msimu huu wakiongozwa na kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck kupenda kutumia mfumo wa kusimamisha mshambuliaji mmoja mbele nayo imechangia timu kuvuna mabao machache katika mechi zake.

Simba ndio timu inayoongozwa kwa kufunga mabao mengi mpaka sasa ikiwa imepachika 10, huku matano yakifungwa na washambuliaji Meddie Kagere na Chris Mugalu waliofunga mawili kila mmoja na John Bocco akifunga moja wakati mengine yakifungwa na viungo Clatous Chama na Mzamiru Yassin waliofunga pia mabao mawili kila mmoja na jingine likifungwa beki Pascal Wawa.

Kwa upande wa Yanga imefunga mabao manne tu, huku mawili yakifungwa na beki Lamine Moro, moja la kiungo Mukoko Tonombe na moja tu la straika Michael Sarpong. Licha ya Yanga kuwa na mastraika wa kimataifa kama Sarpong na Yacouba Sogne wameshindwa kuonyesha uwezo katika mechi hizo huku wadau wengi wa soka wakiwapa muda ili kuona je wanatisha au la. Pia ina Wazir Junior aliyemaliza msimu uliopita na mabao 13 akiwa Mbao FC, msimu huu ameshindwa kupata nafasi ndani ya kikosi cha kocha Mserbia Zlatko Krmpotic.

Kwa upande wa Azam ambayo ndio timu pekee ambayo imeshinda mechi zote nne, imebebwa zaidi na mshambuliaji wao mpya raia wa Zimbabwe, Prince Dube.

Dube ameifungia timu hiyo mabao matatu huku mabao mengine mawili yakifungwa na Obrey Chirwa na Ally Niyonzima hivyo kutimiza idadi ya mabao matano ambayo timu hiyo imefunga hadi sasa.

Timu nyingine kama Namungo washambuliaji wake wapya Sixtus Sabilo na Mghana Steven Sey wameshindwa kuonyesha makali yao ya kuzifumania nyavu katika mechi hizo kama ilivyo kwa wenzao waliopo Dodoma Jiji yenye Peter Mapunda, Michael Chinedu, Khamis Mcha na Dickson Ambundo ama Coastal Union inayoongozwa na mshambuliaji Yusuph Soka aliyekuwa Sweden.

WASIKIE MAKOCHA

Kocha wa Ruvu Shooting, Charles Mkwasa alisema timu zinatengeneza nafasi nyingi lakini tatizo kubwa liko kwa washambuliaji ambao wanashindwa kutumia nafasi hizo.

“Hilo ni tatizo ambalo halipo kwa timu yangu tu bali timu nyingi. Timu zinatengeneza nafasi lakini hazitumiwii ipasavyo hivyo kuinyima timu mabao na wakati mwingine hata ushindi,” alisema Mkwasa.

Kocha wa Biashara United, Francis Baraza alisema tatizo la ubutu wa washambuliaji ni sugu hapa nchini hivyo makocha wana kazi ya kuwaweka sawa kisaikolojia.

“Yaani ni tatizo sugu ambalo sijui linatafutiwaje ufumbuzi. Kila mara tumekuwa tukifundisha mazoezini lakini unakuja kuna muda wanafanya tofauti uwanjani. Hivyo sio kwa makocha tu tunaotakiwa kumaliza tatizo hili bali washambuliaji wenyewe wanatakiwa kujitambua.”