HISIA ZANGU : Simba wamenipa jibu la mgeni, bado Yanga

Tuesday December 3 2019

Simba- wamenipa- jibu -mgeni-bado Yanga-Simba vs Yanga -Azam-uwanja wa kaunda-michezo blog-mwanasport-MwanaspotiSoka-MwanaspotiGazeti-

 

By Edo Kumwembe

UNAPOKUTANA na mgeni anayependa sana soka. Anakuuliza timu zipi ni kubwa nchini. Unamwambia Simba na Yanga. Hii Azam unamtajia baadaye. Imekuja mwaka 2008 tu nadhani. Lazima unamtajia Simba na Yanga. Anakuuliza kitu kingine.

Anakuuliza makao yao. Unamtajia Kariakoo. Anakuuliza ‘Wanafanya mazoezi wapi?’. Unabaki kimya kimya. Unajiuliza kimya kimya moyoni, leo Simba wapo Gymkhana au Bunju Veterani? Unajiuliza ‘Leo Yanga wako Chuo cha Polisi Kurasini au Bunju Veterani?. Unakosa jibu. Unamwambia rafiki yako mgeni ngoja upige simu kuuliza ili kujua wanafanyia wapi mazoezi. Kazi kwelikweli.

Haya ndio maisha ya timu kubwa nchini. Simba na Yanga. Na sasa kupitia picha za mitandaoni, afadhali Simba wanakaribia kupata nyumbani kwao. Itakuwa rahisi mgeni akikuuliza Simba wako wapi, unamjibu tu kwamba ‘Wamejificha kwenye viwanja vyao Bunju’.

Baada ya miaka mingi ya kuponda, hapa najitokeza kuwasifia Simba. Wanachokifanya ni kitu sahihi katika soka. Klabu kubwa na inayotaka mwelekeo haiwezi kukaa Kariakoo. Itatafuta makazi mkubwa ‘ya kujinafasi’ nje ya jiji kwa ajli ya kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.

Yanga wanaweza kujidai kwamba kwa miaka mingi wana uwanja wa Kaunda, lakini ukweli unajidhihirisha kwamba hawawezi kukaa pale. Timu kubwa inapaswa kufanya kile ambacho Azam wamefanya. Unajenga viwanja vilivyoambatana na huduma mbalimbali nje kidogo ya jiji.

Kwa hali ilivyo sasa, hauwezi kupata eneo kubwa katikati ya jiji la Dar es Salaam maeneo ya Posta au Kariakoo na kujenga viwanja viwili vikubwa, Gym, bwawa la kuogelea na mengineo. Ni maeneo kama Bunju au Kigamboni unaweza kufanya hivyo.

Advertisement

Mpira sio kitu cha masikhara kama tunavyokichukulia kwa miaka mingi. Ni maisha ya watu. Ni ajira za watu. Ni utajiri wa watu. Kunahitajika uwekezaji wa hali ya juu. Timu inayojitambua inahitaji viwanja walau vitatu vya mazoezi kwa ajili ya timu ya wakubwa, timu za vijana na watoto pamoja na wanawake.

Moja kati ya biashara nzuri katika soka ni kuuza wachezaji. Wachezaji wanaouzika kwa urahisi zaidi ni wachezaji vijana. Kama timu ya wakubwa haina uhakika na uwanja wa mazoezi, itakuwa vipi kwa timu ya vijana hapo klabuni?

Lakini, hapo hapo Simba na Yanga lazima zijitofautishe na timu nyingine. Kwanini wachezaji wakubwa wanatamani kwenda klabu kubwa duniani? Kwa sababu wanataka kucheza Old Trafford, Anfield, Santiago Bernabeu, Nou Camp na kwingineko. Lakini hapo hapo wanataka kwenda kufanya mazoezi katika viwanja vyao maridadi vya mazoezi.

Lakini leo kulikuwa hakuna tofauti kati ya Simba na Ndanda. Wala Simba na Biashara Mara. Zote hazina viwanja vya mazoezi. Heshima iko wapi? Hakuna. Muda si mrefu heshima itakuwepo kwa Simba. Watu watafahamu ukubwa wao. Kusajiliwa na Simba kutamaanisha kwamba, unakwenda katika viwanja bora vya mazoezi na sio kuvaa jezi nyekundu tu.

Hii ndio heshima walioitengeneza akina Manchester United kwa wachezaji ambao wanatamani kusajiliwa na timu hii kubwa na kufanya mazoezi Carrington. Tofauti ya kusajiliwa na Manchester United au Wigan Athletic unaanza kuiona mapema tu ukifika katika uwanja wa mazoezi kabla haujavaa jezi.

Lakini, hapo hapo klabu inaongoza thamani yake kwa wadhamini. Picha za uwanja wa mazoezi zitakuwa zina mabango mengi ambayo mdhamini ataanza kuiona thamani yake kuanzia katika uwanja wa mazoezi na si vinginevyo.

Kitu kizuri katika hawa rafiki zangu wa Kariakoo ni kwamba, wanapenda kuigana kwa kila kitu. Nimeona rafiki zao wameanza kukata miti kule Kigamboni walikopewa eneo na mheshimiwa mkuu wa mkoa. Ni jambo jema sana.

Siamini kwamba Yanga watakubali kudhalilika kwa muda mrefu wakati watu wakiendelea kuisifia Simba kwa jambo walilofanya. Lazima watahitaji kufanya kitu zaidi kwa ajili ya kuondoka katika makucha ya kusemwa vibaya kwa eneo lao la uwanja wa Kaunda ambalo kwa sasa linaathirika na mafuriko.

Kilichobaki kwa sasa ni kwa majengo yao kuyafanya sehemu ya historia tu. Wanaweza kuingia ubia na makampuni makubwa wakajenga majengo mapya kwa sababu za kibiashara. Timu haiwezi kuweka makao ya kisoka Kariakoo. Inaweza kufanya hivyo Bunju kama Simba walivyo.

Mchezaji hawezi kupata usingizi katika yale majengo ya Msimbazi au Kariakoo. Walau mchezaji anaweza kupata usingizi katika hosteli za kisasa wanazoweza kujenga Bunju au Kigamboni. Ni kama Azam wanavyomaliza mambo yao Chamazi.

Mzee Bakhresa na watoto wake pamoja na utajiri wao wote, lakini hawakulazimisha kununua eneo katikati ya jiji na kuiweka timu maeneo ya Kariakoo au Ubungo.

Walitafuta eneo ambalo linafanana na maeneo ya klabu mbalimbali kubwa barani Afrika ambazo zimewekeza kiukweli kwa ajili ya kutunza timu zao.

Simba wanastahili pongezi nyingi kwa hatua kubwa waliyofikia mpaka sasa. Wanakaribia kutoka eneo moja kwenda jingine na hayo ndio mafanikio. Kuna migogoro mingi ya hapa na pale ndani na uongozi. Lakini hili la viwanja vya uhakika vya mazoezi litabakia kuwa moja kati ya mambo makubwa waliyowahi kufanya katika historia ya klabu yao. Haijalishi nani alinunua ardhi, haijalishi nani alijenga viwanja, wamefanya jambo kubwa kwa klabu yao.

Advertisement