Gwambina yatenga mamilioni kuimaliza Transit Camp FDL

Thursday June 18 2020
gwambina pic

Mwanza. Katika kuhakikisha inacheza Ligi Kuu msimu ujao, uongozi  wa Gwambina FC inayoshriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL), umepanga kutumia Sh 10 milioni kwa ajili ya mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Transit Camp ugenini jijini Dar es Salaam kuhakikisha wanatimiza lengo lao.

Gwambina yenye makao yake wilayani Misungwi mkoani Mwanza, inahitaji pointi tatu tu kati ya mechi nne ilizobakiza kwenye FDL ili iweze kukata rasmi tiketi ya kucheza Ligi Kuu msimu ujap.

Na hilo linaweza kutimia mwishoni mwa wiki ikiwa wataibuka na ushindi dhidi ya Transit Camp, ambao utawafanya wafikishe pointi 43 ambazo hazitoweza kufikiwa na timu nyingine yoyote kwenye kundi Bm

Katibu Mkuu wa Gwambina FC, Daniel Kirai amesema kutokana na umuhimu wa mchezo huo, wameupa kipaumbele kwa kuutengea bajeti maalumu ili kumaliza kazi mapema.

"Nafikiri pesa itaenda nyingi na kwa haraka tunaweza kutumia takribani  Sh 10 milioni kwa sababu huo ni mchezo muhimu ambao utatupa heshima ya kutangaza kupanda Ligi Kuu" amesema Kirai.

Kiasi hicho cha fedha kitatumika katika huduma za kambi, chakula, usafiri, matibabu na gharama za mazoezi katika kipindi chote watakachokuwepo jijini Dar es Salaam hadi mechi hiyo itakapochezwa.

Advertisement

Katibu huyo ameongeza kuwa mbali na bajeti hiyo, wamepanga kutoa motisha kwa wachezaji ikiwamo kuwalipa stahiki zao zote ili wakiingia uwanjani wasiwe na presha yoyote na kwamba kinachowafurahisha viongozi ni ari na morari iliyopo kikosini.

"Hakuna kiongozi yeyote atakayebaki nyumbani wakati wa mechi hiyo, lakini hata mashabiki nao wataanza safari Ijumaa kwa ajili ya kuja kushangilia, huu ni mchezo wa kuandika historia kwa Gwambina FC" amesema Kigogo huyo.

Advertisement