Fundi mwingine atua Yanga

ACHANA kwanza na masharti aliyoanza nayo Cedrick Kaze kwenye matizi ya jana.

Kocha huyo ameshusha mtaalamu mpya wa mazoezi ya viungo tena ni mzawa.

Mtanzania huyo ni Elieneza Nsanganzelu ambaye alikuwa akifanya kazi hiyo pia katika kikosi cha Taifa Stars kwenye benchi la kocha Ettiene Ndayiragije.

Licha ya kwamba vigogo wa Yanga jana walikuwa wagumu kufafanua ishu hiyo, lakini habari za uhakika kutoka ndani ya kambi hiyo Kigamboni zinasema Elieneza ni chaguo la Kaze na alishauriwa kwa karibu na swahiba wake, Ettiene.

Tayari Nsanganzelu yupo kambini Yanga akimaliza wiki sasa na anapiga mzigo. “Alishaanza kazi unajua akiwa kule kwao, (Kaze) aliuliza kama kuna mtaalamu wa mazoezi ya viungo tukamwambia alikuwepo lakini aliondoka mara moja na bado hajarudi akatuagiza lazima aletewe huyo mtu ili aungane na kocha msaidizi wake Juma Mwambusi.

“Haraka tukaona tumtafute Nsanganzelu ambaye alitangulia mapema kambini na kuifanya kazi ya kupandisha ubora wa wachezaji katika utimamu wa mwili na leo (jana) kocha alianza moja kwa moja na mazoezi ya ufundi katika kukisuka kikosi chake,” alidokeza mmoja wa mabosi.

Bosi huyo aliongeza kuwa bado hawajaingia mkataba wowote na Nsanganzelu ambapo walimuomba kwa muda mfupi kuwaimarisha wachezaji baada ya kuondoka kwa Reidoh Bardien ambaye alikuwa akifanya kazi hiyo.

“Hatujaingia naye mkataba tulimuomba tu kwa kipindi ambacho hayupo katika timu ya taifa.”

Kabla ya kutua Taifa Stars, Mwanaspoti linafahamu Nsanganzelu alikuwa akifanya kazi katika kituo cha michezo Symbion akiwa mtaalamu wa mazoezi ya utimamu wa mwili kilichokuwa kikisimamiwa na klabu ya Sunderland ya England. Nsanganzelu alikiri jana kuwa yupo katika kikosi hicho na amekuwa akifanya hivyo katika klabu mbalimbali ikiwemo Azam na KMC ikiwa ni katika kukamilisha programu za mafunzo.

“Itakuwa kuna mtu tu kaniona akajua nimeajiriwa Yanga, mimi bado ni muajiriwa wa TFF, lakini huku kwenye klabu huwa tunapita mara moja moja katika kufanyia kazi programu za mafunzo lakini sio kwamba nimeajiriwa Yanga,” alifafanua Nsanganzelu ambaye habari za ndani zinasema kwamba atakuwa na Yanga kwa muda mrefu kutokana na Kaze kumkubali.

Katika mazoezi ya jana ya Kaze, alianza na mambo madogomadogo ikiwemo kusisitiza staili yake ya mpira pamoja na kuwaambia mabeki na mastaa wengine kwamba anataka mpira wa chini siyo butuabutua.

Kama alivyozungumza na Mwanaspoti kwenye mahojiano maalumu kabla hajatua Tanzania, Kaze jana alikuwa akiwasisitiza wachezaji kwamba anataka timu itawale mpira na ishambulie, muda mwingi mpira uwe kwao na sio wapinzani wao huku ikionekana wazi kwanza kipa Mkenya Faroukh Shikalo ana nafasi kubwa ya kuwa chaguo lake la kwanza.