Fomesheni tatu za Morrison Simba

Wednesday July 22 2020

 

By THOBIAS SEBASTIAN

LICHA ya sakata lake la mkataba na Yanga bado halijapatiwa ufumbuzi, lakini vigogo wa Simba wanasisitiza straika, Bernard Morrison atacheza Msimbazi msimu ujao.

Yanga imeshtakiana na mchezaji huyo kwenye Shirikisho la Soka la Tanzania, ikisisitiza kuutambua mkataba mpya wa kazi wa miaka miwili huku mwajiriwa akiuruka.

Tathmini ya kiufundi ya Simba ya Sven Vandenbroeck inasema wamevutiwa na mchezaji huyo ili kuongeza kasi ya Simba kwenye safu ya ushambuliaji wakitaka aongeze usumbufu kama aliokuwa nao, Emmanuel Okwi enzi zile akiwalaza watu na viatu.

Mfumo wa kwanza ambao Morrison ataingia katika kikosi cha Simba ni ule wa sasa 4-2-3-1, kwa maana ya mabeki wanne, viungo wakabaji wawili, viungo washambuliaji watatu na straika mmoja.

Hapa katika eneo la viungo washambuliaji ndio Morrison anaweza kuingia na akambadili Francis Kahata ambaye sasa anacheza pamoja na Clatous Chama na Luis Jose ambaye licha ya kusajiliwa dirisha dogo ameonyesha kiwango kikubwa.

Kahata anaweza kuchukuliwa nafasi yake kwa sababu kiasilia si mchezaji wa pembeni mwenye uwezo wa kukimbia na kupiga krosi kwa washambuliaji wake kama ambavyo mawinga wengine wanafanya, bali uzuri wake anapokuwa na mpira mguuni ni ngumu kupoteza na kutoa pasi ya maana.

Advertisement

Kwa maana hiyo, Morrison anapata nafasi katika kikosi cha kwanza kwa kumtoa Kahata na akacheza katika nafasi ya viungo watatu akiwa na Chama pamoja na Luis.

4-4-2

Mfumo wa pili ambao Morrison anaweza kuingia katika kikosi cha Simba ni 4-4-2, kwa maana ya mabeki wanne, viungo wanne na washambuliaji asilia wawili.

Simba mfumo huu wameutumia zaidi msimu uliopita kutokana na uwepo wa Okwi akicheza kutokea pembeni lakini ujio wa Sven, mfumo huo hakuutumika tangu alipoumia, Deo Kanda katika mechi ya Yanga, mzunguko wa kwanza kutokana na alikuwa akifiti na kucheza vyema kwenye mfumo huo.

Mfumo wa 4-4-2, mabeki wanne walikuwa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ Shomary Kapombe, Erasto Nyoni na Pascal Wawa, wakati viungo wanne walikuwa Jonas Mkude, Clatous Chama au Sharaf Eldin Shiboub, Deo Kanda na Miraji Athumani au Hassan Dilunga, mastraika John Bocco na Meddie Kagere.

Katika 4-4-2, Morrison anakwenda kucheza katika nafasi mbili ya kwanza kama winga wa kushoto au kulia, kwani ana uwezo wa kupiga chenga mabeki na kuingia kwa nguvu katika boksi na amekuwa na utulivu wa kupiga pasi ya bao na muda mwingine kufunga mwenyewe. Ni mzuri pia kusababisha penalty kama Okwi enzi zile.

Kwa maana hiyo, Morrison anaweza kucheza winga wa kulia wakati kushoto akacheza Luis huku washambuliaji wakiwa Bocco na Kagere au katika mfumo huu wa 4-4-2, anaweza kucheza nyuma ya straika asilia kwa maana nyuma ya straika mmoja ambaye ataanza.

Iko hivi; mawinga wanaweza kucheza Luis na Kahata, wakati huo straika anasimama Bocco au Kagere na nyuma yake ndio akawa Morrison na anaweza kufiti muda mwingine hushuka eneo la kiungo kuchukua mpira, kutengeneza nafasi ya kufunga.

Ni wazi aina ya uchezaji wa Morrison atakwenda kufiti katika mfumo huo wa 4-4-2, jambo ambalo litamfanya kocha wa Simba, Sven kuwa na uhakika wa kumtumia katika nafasi mbili tofauti lakini atafuta mpango na ndoto ya mfalme Okwi kurudi tena msimu ujao kwani aina yao na mahitaji kwa kiasi kikubwa yanafanana.

3-5-2

Simba watafaidika na Morrison katika mfumo mwingine wa 3-5-2, ambao utakuwa na mabeki wa kati watatu, viungo watano na washambuliaji wawili.

Mfumo huu kwa mara ya kwanza Simba waliutumia chini ya kocha, Masoud Djuma kabla ya Mfaransa Pierre Lechantre kutwaa nao ubingwa wa ligi.

Katika msimu huu Sven ameutumia kwenye baadhi ya mechi kama dhidi ya Mwadui alipoaanza na Kennedy Juma, Wawa na Nyoni kwenye viungo watano walikuwepo, Gerson Fraga, Said Ndemla, Luis, Kapombe na Tshabalala ambao walikuwa wanatoka kama mabeki wa pembeni na kucheza eneo la katikati.

Kwenye eneo la ushambuliaji walikuwa wawili Dilunga na Bocco. Morrison anaweza kuingia kucheza katika nafasi tatu tofauti kulingana na mahitaji ya mechi au ambavyo Sven atahitaji.

Morrison anaweza kunoga kwenye kiungo wa pembeni akichukua nafasi ya Dilunga na eneo la kiungo wakawa Fraga, Mkude, Chama, Morrison na Luis au anaweza kucheza kama namba kumi, akachukua nafasi ya Chama na wakawa wamesimama mbele na Bocco.

Sehemu ya tatu ambayo anaweza kucheza ni kama kiungo mshambuliaji nyuma yake akawa Mkude au Fraga wakifanya kazi ya kukaba na kuzuia huku kazi ya kupiga pasi na mipira mingi kwa wachezaji waliokuwa mbele yake Bocco, Kagere, Luis au Kahata akaifanya.

Mchambuzi mahiri nchini, Edo Kumwembe alisema Morrison katika kikosi cha Simba anaweza kuingia katika mifumo yote ambayo kocha Sven atataka kulingana na wapinzani wao walivyo kwani mchezaji huyo ukiondoa tabia zake za nje ya uwanja anasifa nyingi bora ndani ya uwanja.

“Simba wanaweza kumpanga kama kiungo mshambuliaji, winga wa kushoto na kulia, nyuma ya mshambuliaji wa mwisho au hata straika na kote akafiti kwani anauwezo mzuri wa kucheza kwenye maeneo yote hayo bila ya shida yoyote,” alisema.

“Unapokuwa na Morrison hata kama unaenda katika mechi unamkosa Kahata, Luis, Kanda, Chama au mchezaji yoyote ambaye anacheza katika nafasi ya mbele unauhakika upo na mchezaji ambaye atakwenda kuziba nafasi hiyo kama ipasavyo bila shida yoyote,” anasema Kumwembe.

Kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni anasema; “Anaweza akawa anaonekana kama mchezaji mwenye uwezo katika kikosi cha Yanga lakini ubora wa wachezaji aliokutana nao hawatoi ushindani wa kutosha, lakini kama akienda Simba anatakiwa ufanya mara mbili yake kwani kuna wachezaji wenye ubora na hawatakubali nao kuwekwa nje.”

“Akitegemea jina lake na akaanza kubweteka kama ambavyo wamefanya wachezaji wengine waliosajiliwa wakiwa na majina makubwa na wakaishia benchi na atasahaulika.

“Lakini anatakiwa kuwa na tabia nje ambayo itawavutia watu wote ambao wanamzunguka kwani hakuna kocha ambaye anatoa nafasi kwa mchezaji kucheza akiwa na nidhamu mbovu na nategemea akiyafanya hayo atapata nafasi ya kuwika akiwa upande wa pili,” anasema Kibadeni ambaye ndiye mchezaji pekee hadi sasa aliyefunga mabao matatu (Hattrick), peke yake katika mchezo mmoja kwenye mechi za watani wa jadi katika ligi.

Kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ anasema Simba inahitaji wachezaji waliokuwa bora katika usajili wao wa msimu huu ili kwenda kushindana katika mashindano ya kimataifa (Ligi ya Mabingwa Afrika), kwani kwa hapa ndani wameonyesha uwezo mkubwa na hata msimu ujao wanaweza kutwaa mataji mengi zaidi ya ndani.

“Hilo limetokea si kwake tu bali hata kwa Niyonzima ni hivyo hivyo, lakini ukiangalia ubora na uwezo ambao Morrison ameonyesha msimu huu hakuna ambaye anabisha ni mchezaji bora ambaye amekutana na mikasa mingi nje ya uwanja na huenda akiwa mahala penye utulivu atafanya vyema zaidi,” anasema.

“Morrison anaweza kuwa na faida katika kikosi cha Simba kama atakuwa katika kiwango bora anaweza kucheza katika nafasi zote za mbele akasumbuana na walinzi wa timu pinzani na kuhakikisha timu yake inafanikiwa kupitia kwake.

“Lakini mpaka Simba wamefikia maamuzi ya kumsajili basi hayatakuwa namependekezo ya kukurupuka kwani kocha wao watakuwa wamemuhusisha na amekubali hilo kwa maana hiyo naona nafasi ya nyota huyo kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza kwa hakuna mwalimu ambaye anamsajili kwa mapendekezo yake mchezaji fulani halafu amuweke nje labda awe ameletewa,” anasema Julio ambaye amewahi kuzifundisha Mwadui na Coastal Union.

“Kuhusu tabia ya Morrison hiyo inaweza kubadilika kutokana na maadili ambayo atayakuta katika timu kama atafanikiwa kubanwa na kutoishi kwa uhuru,” aliongezea Julio.

TABIA

Miongoni mwa mikasa ambayo Morrison amepitia kwa muda mfupi akiwa ndani ya kikosi cha Yanga ni utovu wa nidhamu ndani na nje ya uwanja ingawa Simba wanadai amekuwa akifanya hivyo kutokana na kulegea kwa sehemu ya uongozi wa Yanga.

Ukiachana na mikasa hiyo ya utovu wa kinidamu kwa Morrison alionyesha tena lingine waziwazi katika mechi ya Simba mara baada ya kutolewa aliondoka moja kwa moja nyumbani kwake wala hakukaa katika benchi la wachezaji wa akiba wala katika vyumba vya kubadilishia nguo ya timu hiyo.

Katika mkuu wa zamani wa TFF, Angetile Osiah anasema mchezaji huyo ni mzuri lakini anapaswa kudhibitiwa nidhamu yake kwa maandishi kwavile amekuwa na mambo ya kujirudia.

NAFASI YAKE YANGA

Morrison kwa muda wa nusu msimu aliokuwa katika kikosi cha Yanga amekuwa mchezaji wa kutegemewa na kucheza katika kikosi cha kwanza ukiachilia mbali wakati ambao alikuwa akipitia mikasa mingi kama ilivyo sasa na hilo limetokea kwake kutokana na ubora wa maeneo mengi.

Katika kikosi cha kwanza Yanga, Morrison pindi anapokuwa uwanjani alikuwa akihusisha kutengeneza nafasi za kufunga, anafunga mwenyewe, anauwezo wa kumiliki mpira na kufanya vitu vya madaha ambavyo vimewafanya hata mashabiki wa timu hiyo kuwa kipenzi chao.

Mashabiki wa Yanga wamekuwa wakivutiwa na Morrison kutokana na umahiri wake na kitu ambacho hawawezi kukisahau kwake ni kuifunga Simba katika mechi ya pili ya Ligi Kuu Bara kwa faulo.

Bao hilo liliwapa Yanga kiburi mtaani kwa muda mrefu kabla ya kufungwa na Simba mabao 4-1 kwenye kombe la FA.

Advertisement