Fabregas ataja wachawi waliomvua jezi Chelsea

Muktasari:

  • Fabregas alicheza mechi sita tu za Ligi Kuu England kwenye kikosi cha Chelsea msimu huu kabla ya kuaondoka huku akisema malengo yake yalikuwa kupata timu itakayompa nafasi ya kucheza kila mechi na ndio maana ametimkia zake Ufaransa.

MONACO, UFARANSA.KIUNGO fundi wa mpira, Cesc Fabregas amesema ameamua kuihama Chelsea na kutimkia zake Monaco kwa sababu tu ya ujio wa kocha Maurizio Sarri na kiungo Jorginho kutoka Napoli huko Stamford Bridge mwaka jana.

Fabregas , ambaye amecheza Chelsea kwa miaka minne na nusu baada ya kutua Stamford Bridge akitokea Barcelona mwaka 2014, alijiunga na miamba ya Ligue 1 kwenye dirisha la Januari mwaka huu baada ya kushindwa kupata nafasi chini ya kocha Sarri.

Mhispaniola huyo siku zake zilianza kuhesabika baada ya kuja Jorginho, ambaye kimsingi watu wanamwita mtoto wa Sarri kutokana na kumpanga hata kama hachezi kwenye ubora unaotakiwa. Kiungo huyo alitua Stamford Bridge kwa ada ya Pauni 50 milioni.

“Napenda kuwa na majukumu mapya. Muda wote kwangu mimi ni muhimu kuwa na malengo mapya,” alisema Fab.

“Nilikuwa Chelsea na ningeweza kusaini mkataba mpya na kubaki pale, lakini kocha mpya alikuwa na mchezaji ambaye kama mwanaye.”

Fabregas alicheza mechi sita tu za Ligi Kuu England kwenye kikosi cha Chelsea msimu huu kabla ya kuaondoka huku akisema malengo yake yalikuwa kupata timu itakayompa nafasi ya kucheza kila mechi na ndio maana ametimkia zake Ufaransa.

Tangu alipotua Monaco na kusaini mkataba wa miaka mitatu na nusu Januari mwaka huu, Fabregas amefunga bao moja katika mechi 11 alizocheza kwenye Ligue 1 huku timu hiyo ikipambana isishuke daraja.