Eymael ataka mabao 16 fasta fasta Yanga SC

Saturday March 21 2020

Eymael ataka mabao 16 fasta fasta Yanga SC,BENCHI la ufundi la Yanga, chini ya kocha Luc Eymael ,

 

By Charles Abel

BENCHI la ufundi la Yanga, chini ya kocha Luc Eymael limeanza kufanya hesabu za mbali, ambapo limeanza kudokeza kwa viongozi baadhi ya majina ya wachezaji ambao wameshauri wamalizane nao haraka kama inawezekana.

Yanga itatumia kipindi hiki cha mapumziko kufanya mazungumzo na ikiwezekana kumalizana na nyota wawili wanaocheza katika nafasi ya ushambuliaji, Sixtus Sabilo wa Polisi Tanzania na Reliants Lusajo wa Namungo FC ambao wote kwa ujumla mpaka sasa wamepachika mabao 16 kwenye Ligi Kuu ya Bara.

Mmoja wa vigogo nyeti kwenye usajili wa Yanga alisema kwamba kocha amewaambia kwamba mastaa hao wana sifa za kucheza Yanga msimu ujao na mpaka umri unaruhusu.

“Kocha amekuwa akifuatilia baadhi ya wachezaji wazawa na ambao amesisitiza tuhakikishe wanapatikana ni Sabilo yule anayechezea Polisi Tanzania na Lusajo wa Namungo.

“Hao ndio wazawa ambao anaona wako fiti na wanaweza kumpa kile anachokihitaji kwani anataka awe na mshambuliaji mwenye uwezo wa kufumania nyavu, kasi na pia kuchezesha timu na hizo sifa zote Lusajo na Sabilo wanazo.

“Lusajo amemuona ni mtu anayeweza kukaa katika nafasi na ana uwezo mkubwa wa kutumia pasi za mabao anazopewa lakini pia ana uwezo wa kupiga pasi za mwisho na Sabilo mbali na kufunga, anaweza kuchezesha timu na kupika mabao kwa wenzake,” alisema kiongozi huyo.

Advertisement

Mwanaspoti linafahamu kwamba mara baada ya msimu kwisha, Sabilo atakuwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake wa miezi sita na Polisi Tanzania wakati Lusajo ana mkataba wa mwaka mmoja na Namungo FC ambao utaisha mwisho wa msimu huu.

Lusajo amekuwa moto wa kuotea mbali tangu alipojiunga na Namungo FC mwaka 2018 akitokea Dodoma Jiji FC aliyojiunga nayo kutokea Toto Africans. Katika msimu wa 2018/2019, Lusajo alitoa mchango mkubwa katika kuipandisha Namungo FC, Ligi Kuu baada ya kuifungia mabao 16 katika Ligi Daraja la Kwanza. Na msimu huu, ameshafunga mabao 11 katika Ligi Kuu ambayo yanamfanya awe mzawa aliyefunga idadi kubwa ya mabao huku pia akipiga pasi tatu zilizozaa mabao.

Kwa upande wa Sabilo, amefunga jumla ya mabao sita na kupiga pasi tatu za mwisho akichangia kuifanya Polisi Tanzania iwe katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi. Mshambuliaji huyo wa zamani wa Stand United, aliachana na KMC baada ya benchi la ufundi la timu hiyo kuonyesha kutoridhishwa na kiwango chake.

Advertisement