Dodoma FC yahamishia majeshi yake Gairo

Muktasari:

Pamoja na mabadiliko hayo, alisema uongozi unawaomba mashabiki wa timu wasiache kujitokeza kwa wingi mjini Gairo ili kuwaongezea morali wachezaji kwenye mchezo huo muhimu.

UONGOZI wa Dodoma FC umehamishia majeshi yake kwenye Uwanja wa CCM Gairo ikiwa siku chache baada ya Mtibwa Sugar kutangaza kuutumia uwanja huo kwenye michezo yake ya Ligi Kuu.

Taarifa iliyotolewa na timu hiyo imeeleza utatumia uwanja huo kwa muda katika michezo yake ya nyumbabni ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inayoendele kesho Jumamosi na wataikaribisha Mlale FC.

“Mabadiliko haya ya uwanja, yamesababishwa na muingiliano wa ratiba katika uwanja wetu wa nyumbani wa CCM Jamhuri na uwanja huo kwa sasa una matumizi mengine ya kijamii,” ilieleza taarifa hiyo iliyotolewa na idara ya mawasiliano ya timu.

Hata hivyo, Katibu wa timu hiyo, Fortunatus John alisema uongozi unaomba radhi kwa mashabiki na wapenzi wote wa soka wa Jiji la Dodoma kutokana na mabadiliko hayo ambayo yatawanyima fursa mashabiki wengi kuiona timu yao ikicheza uwanja wa nyumbani.

Pamoja na mabadiliko hayo, alisema uongozi unawaomba mashabiki wa timu wasiache kujitokeza kwa wingi mjini Gairo ili kuwaongezea morali wachezaji kwenye mchezo huo muhimu.

Alisema uongozi kwa kushirikiana na wamiliki wa uwanja unaahidi kufanya jitihada kubwa ili kuondoa kasoro zilizojitokeza na kuhakikisha mchezo wetu ujao dhidi ya Majimaji FC ya Ruvuma unafanyika katika uwanja wa nyumbani wa CCM Jamhuri uliopo jijini Dodoma.