Depay: Sielewi Barca walikwama wapi

Amsterdam, Uholanzi. OLYMPIQUE Lyon na Barcelona zilikuwa kwenye hatua za mwisho kufanya biashara tamu ya Memphis Depay. Nahodha huyo wa Lyon kwa sasa yuko kwenye kiwango bora kabisa na Kocha wa Barcelona, Ronald Koeman akaawambia mabosi zake waende wakafanye biashara kumpeleka Nou Camp.

Hata hivyo, kilichotokea hata Depay mwenyewe kimemshangaza kwani, alikuwa akisubiri dili hilo kutimia ili aende zake kucheza na supastaa matata kabisa wa dunia, Lionel Messi.

Lakini, dili hilo likakwama saa chache kabla ya dirisha la usajili kufungwa huku Manchester United ikitajwa kukwamisha mambo kimtindo.

Awali, Barcelona na Manchester United walikuwa kwenye mazungumzo ya kumpeleka Ousmane Dembele kwa mkopo pale Old Trafford hadi mwishoni mwa msimu.

Hata hivyo, baadaye Barcelona wakageuza kibao na kutaka kumuuza jumla ili kupata fedha za kumnunua Depay kwa dau la Pauni 25 milioni, lakini Man United hawakuwa tayari kumnunua jumla kwa sasa kutokana na mtikisiko wa kiuchumi sababu ya corona.

Lakini, Depay mwenyewe amesema kwamba hafahamu nini kimetokea hadi dili hilo kushindwa kukamilika licha ya kuwa ana furaha kuwepo Lyon. Alisema kuwa Barcelona ni timu ya ndoto yake na licha ya dili kukwama kwa sasa, lakini hajakata tamaa akiamini akipambana kwa bidii kuna siku atavaa jezi ya wababe hao.

“Sifahamu nini kimetokea, lakini imepita kama ilivyopita na naendelea kufurahia maisha ya hapa. Natambua nina wajibu wa kufanya kazi kwa bidii ili kuisaidia Lyon na mambo mengine yatajulikana hapo baadaye,” alisema Depay na kuongeza: Huenda ikawa ngumu kwa nafasi kama ile kutokea tena ila jambo la msingi ni kukuza kiwango na ofa zitakuja tu.”

Depay alijiunga na Lyon mwaka 2017 baada ya kuonyesha kiwango kibovu akiwa na Man United wakati akipewa nafasi kubwa ya kutisha na wababe hao wa Old Trafford.