Corona? Huko Belarus kinawaka tu

Muktasari:

Katika mchezo huo, Energetik BGU iliwachapa wapinzani wao BATE Borisov kwa mabao 3-1 kwenye mechi ya ufunguzi huku Rais wa FA, Vladimir Bazanov akisisitiza ligi hiyo itaendela kama ilivyopangwa.

BATE, Belarus . WAKATI ligi karibu zote duniani zikisimama kupisha janga la kusambaa kwa virusi vya corona, lakini kuna taifa moja mambo yanaendelea kama kawaida tu.

Yaani hawafahamu kitu kuhusu Corona na Rais wa nchi hiyo amesema moja ya njia za kukabiliana na janga hilo ni kuwa imara.

Ndio, juzi kwenye uwanja wa Misnk kukapigwa mechi moja kali ya Ligi Kuu ya nchi hiyo maarufu kama Vysheyshaya Liga huku mashabiki wakifurika uwanjani kama kawaida.

Katika mchezo huo, Energetik BGU iliwachapa wapinzani wao BATE Borisov kwa mabao 3-1 kwenye mechi ya ufunguzi huku Rais wa FA, Vladimir Bazanov akisisitiza ligi hiyo itaendela kama ilivyopangwa.

“Kwa sababu gani tusianze ligi…kwani kuna janga la kitaifa kwenye nchi yetu? Hakuna tishio lolote kwa sasa na tumeamua michuano itafanyika kwa wakati na tunaanza leo,” alisema bosi huyo wa FA.

Hata hivyo, tofauti na mataifa mengine ya Ulaya, Belarus ina waathirika 81 wa corona ambao wamethibitishwa kuwa na virusi hivyo. Mwathirika wa kwanza alibainika Februari 28, mwaka huu na hatua mbalimbali zimechukuliwa.

Lakini, imeelezwa kuendelea kuwepo kwa michezo na mikusanyiko ya watu kunaweza kusambaza virusi hivyo.

Hata hivyo, kwa upande wa Bazanov mawazo yake ni tofauti kabisa ambapo, alisema:

“Ndio, ligi nyingi kwenye nchi za Ulaya mechi zimekuwa zikiendelea bila mashabiki. Lakini, mashabiki huonekana wamezunguka nje ya viwanja hivyo, kufanya hatari kuwa pale pale tu.”

Rais wa nchi hiyo, Alexander Lukashenko amesema kila kitu kiko wazi na kwamba, hakuna sababu ya kuwa na hofu na watu waendelee kufanya kazi.