Coastal warejea kuvutia kasi upyaa

Tuesday September 15 2020

 

By SADDAM SADICK

KUFUATIA matokeo yasiyoridhisha katika kikosi cha Coastal Union, beki wa kushoto wa timu hiyo, Hans Masoud amekiri kuwa Ligi Kuu ni ngumu hasa mechi za ugenini na kwamba, wanarudi nyumbani Tanga ili kufanya kweli dhidi ya Dodoma Jiji.

Coastal Union imeanza vibaya msimu kutokana na kupoteza mechi mbili mfululizo ilizoanzia ugenini ikiwa ni dhidi ya Namungo walipofungwa bao 1-0 kisha kulala 2-0 mbele ya Azam.

Msimu uliopita ‘Wagosi’ hao walimaliza ligi katika nafasi ya saba wakiwa na pointi 53, huku ikiwa ni moja ya timu iliyoonyesha soka la ushindani na nidhamu chini ya Kocha Juma Mgunda.

Masoud alisema ligi imeanza na ushindani mkali hasa timu nyingi kutumia vyema viwanja vyao vya nyumbani na kwamba, hawataki kufikiria yaliyopita isipokuwa wanajipanga na mechi ijayo.

Alisema kutokana na matokeo waliyopata ugenini ambayo yanawaumiza vichwa, kwa sasa wanarudi nyumbani kujiandaa na mchezo dhidi ya Dodoma Jiji FC ili kusahihisha makosa.

“Timu nyingi zimetumia faida ya nyumbani kupata ushindi, sisi tulianzia ugenini na sasa tunaenda nyumbani ambapo na tutapambana kupata ushindi na kurejesha nguvu mpya,” alisema Masoud.

Advertisement

Beki huyo wa zamani wa Alliance FC, aliongeza kuwa licha ya kuuanza vibaya msimu, lakini sio kwamba wanacheza chini ya kiwango, isipokuwa ni bahati kutokuwa upande wao na kwamba watabadilika na kufanya vizuri.

“Naamini wengi wanaona kiwango chetu, sio kwamba tunacheza vibaya isipokuwa bahati haikuwa upande wetu, lakini tunaamini katika mwendelezo wa ligi tutabadilika na kufanya kweli.”

Advertisement