Cheki picha la Morrison mabosi huko Simba, Yanga wazungukana

Sunday June 14 2020

 

By THOBIAS SEBASTIAN

YANGA wamegundua kuna kitu kinaendelea baina ya straika wao, Bernard Morrison na baadhi ya watu wa Simba.

Morrison hakuwepo kwenye kikosi cha Yanga kilichowavaa Mwadui jana mjini Shinyanga, baada ya kuwazimia simu viongozi siku ya kuondoka Ijumaa asubuhi huku akiwaambia wenzake kwamba, bado ana hofu na virusi vya corona.

Awali, nyota huyo aliyekaa kwenye mioyo ya mashabiki wa Yanga baada ya kuwafunga Simba, aligoma kusafiri kwa basi na wenzake lakini hata alipopewa tiketi ya ndege akaingia mitini.

Mmoja wa vigogo wa Yanga ameliambia Mwanaspoti mjini Shinyanga kwamba;”Tumesikia kuna watu wa Simba bado wanamsumbua sumbua wanamtajia pesa nyingi kwamba, aende kusaini kwao, sasa kinachotushangaza sijui anasahau kuwa ana mkataba wa miaka miwili na Yanga na hili analofanya tunasubiri awashe simu atuambie, maana huu ni utovu wa nidhamu.

“Sasa tunaanza kuona usumbufu wake, lakini tusiseme mengi acha tusubiri kwani hata kama simu yake inashida klabu anaijua na ofisi za viongozi anazijua, unauliza kwamba labda anadai mishahara? Hakuna mchezaji anayedai mshahara labda ni wa mwezi wa sita na kuendelea wakati wa kuwalipa haujafika,” alisema huku akidai kwamba kuna habari wamezisikia kuwa kuna kigogo mmoja wa Simba alimpa mchezaji huyo kishika uchumba cha dola 10,000 (Sh23milioni).

Mkataba wa miezi sita wa Morrison na Yanga unaelekea ukingoni na tayari walishasaini mkataba mwingine wa miaka miwili zaidi ambapo, Mwanaspoti linafahamu kuwa tayari mkataba huo upo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ingawa inadaiwa kwamba, haujakamilika katika baadhi ya makubaliano na hapo ndipo Mghana huyo ameanza kuwashika pabaya. .

Advertisement

Habari zinasema kwamba Simba wamemhakikishia mchezaji huyo maisha ndiyo sababu amekuwa akipagawa ingawa Yanga watamuwekea kikao kizito wakisharejea Dar es Salaam kujua tatizo ni nini.

Habari zinasema kwamba Simba wanatamani kuwa na Morrison kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao ingawa na Yanga nao wameiambia Mwanaspoti kwamba, wanasubiri kuona picha linavyokwenda huku wakijiaminisha kuwa Simba itachemka mapema tu.

Kinachowapa kiburi Yanga na ushikaji wa Morrison na GSM ambao wanajua kinachoendelea ingawa wamepagawa zaidi baada ya kusikia kwamba, Pappy Tshishimbi naye bado yupo kwenye rada za Simba kama ilivyo kwa beki wa Coastal Union, Bakari Mwamnyeto.

Yanga walishafanya mazungumzo ya awali na Papy lakini bado mambo hayajaisha huku Mwamnyeto wakisubiri wakala wake atue kutoka Italia na walishampelekea mchezaji mkataba wa awali.

Mwanaspoti baada ya kupata mchezo mzima lilimtafuta Morrison, ambaye hakuwa na maneno mengi zaidi ya kueleza kwa ufupi “Nipo nimetoka katika mazoezi yangu binafsi kwenye fukwe za bahari ili kuwa fiti na kuhusu masuala ya kuondoka Yanga na kwenda timu nyingine hayo ni ya uongozi.”

Habari za ndani ya Yanga zinasema kwamba wenzao wa Simba wamekuwa wakiwatingisha kwamba, wana picha za Morrison akisaini kwa Mwenyekiti wao, Mohammed Dewji MO.

MO ‘alitweet’ wiki moja iliyopita kwamba kuna kishindo kinakuja na kuwa hawako kimya, wanaelewa kila kinachoendelea ingawa hakufafanua kwa undani.

Mwanaspoti lilimtafuta Tshishimbi na kueleza kuwa hata kama mkataba wake unamalizika nafasi ya kwanza anaipa timu yake ya Yanga kwani, kwa muda wote aliokuwepo nchini ameishi nao vizuri kwa upendo.

Mkurugenzi wa GSM, Hersi Said alieleza kwa upande wao wana nguvu ya kutosha kwa maana ya kiuchumi ya kuwabakisha wachezaji wao ambao, wanamaliza mikataba ambao watakuwa wamependekezwa na benchi la ufundi na kusajili wengine wapya ni ishu ya muda tu.

Ofisa habari wa Simba, Haji Manara alieleza kuwa mwisho wa msimu watafanya kishindo katika usajili ambacho kuna mashabiki wa timu fulani watapelekwa hospitali kwa presha.

“Hiki kishindo ambacho tutakifanya katika usajili kitakwenda kushtua, lakini kwamba Simba tunamtaka Morrison hilo si la kweli na kuna watu wanazusha,” alisema Manara.

Advertisement