Chama: Nitasaini Simba Sc

BAADA ya kuenea kwa maneno mengi mitandaoni, staa wa Simba, Clatous ameliita Mwanaspoti nyumbani kwake na ‘kulihutubia taifa’. Ameweka sawa mambo kibao ili Taifa na umma wa Wanasimba kupitia Mwanaspoti uelewe ukweli na masuala yanavyoendelea juu yake na klabu hiyo, pamoja na zingine zinazohusishwa naye.

Amezungumza mambo kibao ya maana, lakini mojawapo ni hili, “asilimia 80 mpaka sasa nasaini Simba, Yanga watanisamehe.”

Staa huyo ambaye ni nadra kuzungumza na vyombo vya habari amelipa heshima Mwanaspoti pekee na kukiri kwamba kumekuwa na mambo kibao ambayo yamekuwa yakiendelea na ameona ni bora kuyaweka sawa ili umma uelewe kwamba soka ni kazi yake.

Chama ambaye ni raia wa Zambia, anasema kwamba ana uhakika pamoja na dau ambalo Yanga wamemuahidi kupitia wakala wake, bado ana deni la kuendelea kuwatumikia Simba kwa miaka mingine miwili kama walichozungumza watakubaliana na akasaini. Pamoja na hilo, endelea kutiririka naye.

MKATABA SIMBA

Chama anasema mkataba wake na Simba unamalizika mwisho wa msimu huu na wameanza mazungumzo ya kuongeza mpya wa miaka miwili ambao utakuwa na masilahi zaidi ya aliyokuwa akipata hapo awali.

“Mazungumzo yangu na viongozi wa Simba juu ya kuongeza mkataba mpya yanakwenda vizuri na kuna mambo katika masilahi nimeomba waniongezee kama ambavyo nimekuwa nikihitaji ili niweze kusaini (mkataba) mpya jambo ambalo linakwenda vizuri bila wasiwasi wowote,” anasema.

“Kama mambo hayo yatakwenda vizuri na naamani viongozi wa Simba wamekubaliana nami, siku sio nyingi nitasaini mkataba mpya kama ambavyo nimekuwa nikieleza katika maeneo mbalimbali mashabiki wa Msimbazi wanaponiuliza suala hili.

“Niwatoe hofu mashabiki wa Simba, nina asilimia zaidi ya 80 kusaini mkataba na Simba ili kuendelea kuwa hapa kwa miaka miwili mingine zaidi na kama ikitokea hilo likishindikana sitacheza timu nyingine hapa Tanzania.”

Chama anasema kuna mmoja wa mawakala anayeishi Zambia wakati alipokwenda likizo wiki iliyopita alikutana naye na kumueleza kuwa kuna timu inaitwa

Yanga inatokea Tanzania inahitaji huduma yake kwa dau nono.

“Wakala ni kweli alimpigia mmoja wa mabosi wa Yanga video call ili kumuonyesha kuwa yupo na mimi na tunazungumza dili la kwenda kucheza katika klabu hiyo mara baada ya mkataba wangu kumalizika mwisho wa msimu huu.

“Baada ya hapo huyo wakala aliniambia dau ambalo Yanga wameliweka mezani, lakini akifanikisha tu mimi kuonana na Yanga kuna kiasi cha fedha atachukua na akifanikisha mpango na kusaini timu hiyo atachukua kiasi kingine kikubwa cha pesa ambacho ni zaidi ya awali.

“Wala sikutaka kuzunguka nilimueleza wakala huyo bado nipo na mkataba na Simba na hata asifikirie kama naweza kukubali kusaini mkataba, lakini hata huyo kiongozi ambaye alikuwa anaongea hapo alitaka kuja Zambia asije maana hataweza kuonana nami au hatanikuta kabisa,” anasema Chama na kudai kwamba dau la Yanga aliloambiwa na wakala huyo ni zaidi ya Sh400 milioni.

“Kabla ya Simba kuongea lolote kiukweli kwa mambo ambayo wamenifanyia kwa muda wote wa miaka mitatu niliyocheza soka kwao wamenifanya kuwa na vitu vingi ambavyo sijawahi kuvipata huko nyuma katika maisha yangu ya soka, kwa maana hiyo nitawapa heshima kubwa.

“Heshima ambayo nitawapatia Simba kama tutashindwa kukubaliana katika mkataba mpya kiukweli sitakubali kwenda Yanga wala timu nyingine yoyote hapa Tanzania iwe Azam, Mtibwa Sugar au nyinginezo, nitaondoka kwenda nyumbani Zambia kutafuta timu ya kucheza au nchi nyingine.”

HESHIMA YANGA

Kiungo huyo mwenye utulivu anapokuwa uwanjani anasema mbali ya kuonyesha dhamira ya dhati kuongeza mkataba mpya Simba, anatoa heshima kwa Yanga ambayo imeonyesha nia ya kumhitaji na kuweka pesa nyingi mezani ambazo kwa maisha ya wachezaji wa Afrika sio rahisi kuacha kuzichukua.

“Nawaheshimu sana, sana, Yanga ni timu kubwa ambayo ina wachezaji wazuri na viongozi wenye weledi katika soka, lakini mambo ambayo Simba wamenifanyia kwa muda wa miaka mitatu ni ngumu kuondoka kwao na kwenda kucheza timu nyingine ya hapa nchini.

“Ushindani uliokuwepo baina ya Simba na Yanga halafu niondoke nilipokuwa ili kwenda kwao nitawaumiza viongozi walionileta hapa nchini, hata wale mashabiki ambao walikuwa wanaonyesha upendo wa dhati juu yangu katika vipindi vizuri na vibaya ambavyo nimepitia hapa.

“Mpira ni mchezo ambao unahusisha pesa ili wachezaji tuendeshe maisha yetu pamoja na familia au watu ambao wanatutegemea, ndio maana nimewapa heshima Yanga kwa kutambua hilo na kuweka pesa ya kutosha,” anasema Chama ambaye amekuwa akihitajiwa na timu hiyo tangu msimu uliopita.

UNAJUA KUNA KITU GANI AMEPANIA KUFANYA HIVI KARIBUNI? SAPRAIZI GANI ANAYO?

USIKOSE MWENDELEZO WA MAHOJIANO YAKE KESHO KWENYE MWANASPOTI.