Cameroon vidume Afcon U-17

Monday April 29 2019

 

By Thomas Ng'itu

WABEBA tena. Ndio, Cameroon jioni ya jana walinyakua taji la Afcon U17 2019 kwa mara ya pili baada ya kuinyuka Guinea kwa mikwaju wa penalti 5-3 kwenye mechi ya fainali baada ya kutoka suluhu dakika 90.

Cameroon ilinyakua taji la kwanza la fainali hizo za Vijana mwaka 2003 na ubingwa wa jana umeifanya ilingane na Ghana, Nigeria na Mali kwa kutwaa mara mbili kila moja tangu Afcon U-17 kuanza mwaka 1995.

Katika dakika 90 za pambano hilo lililopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na kuhitimisha wiki mbili za fainali hizo zilizofanyika kwa mara ya kwanza Tanzania, timu hizo zilishindwa kufungana huku kila upande ukipoteza nafasi za wazi.

Cameroon ilipata penalti zake kupitia kwa nahodha wake; Steve Mvoue aliyenyakua tuzo ya Mchezaji Bora wa michuano hiyo, Ndongo, Wamba Djouffo, Nang na Alioum, huku Bangoura, Toure na Conte wakiifungia Guinea na mkwaju wa Sacko ukipanguliwa na kipa wa Cameroon, Manfred Ekoi.

Naye Straika wa Angola, Osvaldo Capemba akiibuka Mfungaji Bora akitupia nyavuni mabao manne na Mvoue wa Cameroon akiibuka Mchezaji Bora wa Fainali hizo za 2019.

Washindi wa fainali hizo ikiwamo Guinea iliyomaliza ya tatu, Angola walitwaa ushindi wa tatu walikabidhiwa zawadi zao na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza aliyekuwa Mgeni rasmi wa fainali hizo.

Advertisement

Timu hizo zote tatu pamoja na Nigeria waliomaliza wa nne wamefuzu Fainali za Kombe la Dunia za Vijana U-17, 2019 zitazofanyika Brazil baadaye Oktoba katika tarehe itakayotajwa.

Advertisement