Buriani Dk Paul Marealle

Muktasari:

Katika Shirikisho la Soka (TFF), daktari huyu bingwa wa mifupa kapiga kazi na marais watatu, awamu tatu akiwa mjumbe wa kamati tendaji

Ni majonzi. Si kwa wale tu tuliofanya kazi na Dk Paul Gaspar Marealle (59), bali kwa familia na wadau wa mpira wa miguu ndani na nje ya Tanzania.

Niko kwenye shughuli za mpira wa miguu kwa muda mrefu. Moja ya vitu vizito kwangu kufanya ni kuandika tanzia inapokea Mwenyezi Mungu amempenda zaidi mmoja kati ya wanafamilia wenzangu wa mpira wa miguu.

Nakumbuka huko nyuma nimewahi kuandika tanzia kwa wanafamilia wawili tu wa mpira wa miguu walioitwa na Muumba wao; aliyekuwa Katibu Mkuu wa zamani wa kilichokuwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) sasa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Kanali Ali Hassan Mwanakatwe, na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Epaphra Amana Swai.

Ni ngumu kuandika tanzia kwa vile nafanya hivyo nikiwa na majonzi, lakini rohoni nasukumwa kuwa ni lazima niandike kitu kwa vile aliyetangulia mbele ya haki alikuwa mmoja wa watu wa karibu kwangu katika masuala ya uendeshaji mpira wa miguu.

Desemba 14, mwaka huu, saa 3.30 asubuhi napata ujumbe mfupi wa maneno kupitia WhatsApp kutoka kwa Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred kuwa Dk Paul Marealle amefariki dunia usiku wa saa 4 (Desemba 13, 2020). Hivyo, tuwaandikie Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) juu ya msiba huo.

Haraka kumbukumbu zangu zinarudi mwanzoni mwa mwezi huu nilipokuwa kikazi jijini Arusha. Huko nilikutana na Dk Joseph Kabungo kutoka Zambia ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Tiba ya CAF. Dk Marealle mbali ya kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, alikuwa pia Mjumbe wa Kamati ya Tiba ya CAF.

Dk Kabungo alizungumza nami kuhusu Dk Marealle ambaye wakati huo alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI). Moja ya vitu alivyozungumza Dk Kabungo ni kuwa Dk Marealle ni mtu mnyenyekevu na mwepesi wa kushirikiana na kila mtu na anamuombea nafuu ya haraka. Nilifahamiana na Dk Marealle tangu mwaka 2013 baada ya daktari bingwa huyo wa mifupa kuteuliwa na Rais wa TFF wakati huo Leodegar Tenga kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji na moja kwa moja kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Tiba ya TFF. Wakati huo nilikuwa Ofisa Habari wa TFF.

Dk Marealle alipokea kijiti cha kuongoza Kamati ya Tiba ya TFF baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, na daktari bingwa wa mifupa Dk Sylvester Faya kuomba kupumzika.

Tangu wakati huo, Dk Marealle alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji akiongoza Kamati ya Tiba hadi anafariki. Aliifanya kazi hiyo kwa weledi, na ndiyo maana haikushangaza hata baada ya uongozi wa Rais Tenga bado aliteuliwa na Rais Jamal Malinzi, na baadaye Rais Wallace Karia.

Mara ya mwisho kufanya kazi kwa ukaribu na Dk Marealle ni kipindi cha mlipuko wa janga la Covid-19. Eneo tulilolifanyia kazi kwa pamoja ni kuweka katika lugha rahisi kwa wadau wa mpira wa miguu Kanuni za Covid-19 zilizoandaliwa na Serikali baada ya kuruhusu kuendelea kwa ligi.

Moja ya eneo ambalo nilikuwa na majadiliano ya kina na Dk Marealle ni kipindi ambacho kulikuwa na malalamiko mengi kuwa vyumba katika baadhi ya viwanja vilikuwa vikipuliziwa dawa ili kuathiri wachezaji wa timu pinzani. Wakati nikiwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, nilimtaka Dk Marealle kupitia kamati yake ya Tiba wafanyie uchunguzi madai hayo.

Mara zote Dk Marealle, tena kwa ucheshi alipinga hilo kwa maelezo kuwa wanaodai hivyo hawawezi kutoa uthibitisho wowote wa kisayansi kuthibitisha madai yao. Alisema labda vyumba vya kubadilishia vina changamoto nyingine, lakini si kupuliziwa dawa.

Maelezo yake yalinifanya nipange safari ya kimya kimya kwenda mjini Shinyanga kukagua Uwanja wa Kambarage katika moja ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom, kwani ndiyo uliokuwa ukilalamikiwa mara kwa mara. Baada ya ukaguzi niligundua madirisha ya vyumba hivyo ni madogo na yako kwa juu, hivyo hayaingizi hewa ya kutosha.

Baada ya ukaguzi huo, niliwaelekeza wamiliki wa uwanja huo waongeze ukubwa wa madirisha, jambo ambalo walilitekeleza. Tangu hapo hakukuwa tena na malalamiko dhidi ya Stand United kuwa wanapuliza dawa vyumbani. Kama alivyoniambia Dk Kabungo, Dk Marealle alikuwa mnyenyekevu na rahisi kufanya kazi na yeyote. Lakini vilevile Dk Marealle alionesha weledi katika fani yake kwa mara zote kusisitiza umuhimu wa tiba si kwa wachezaji tu, bali hata sisi wengine tuliokuwa tumemzunguka.

Kutokana na changamoto ya maumivu ya mgongo ambayo niliwahi kupata, nilipata fursa ya kuhudumiwa na Dk Marealle kwa dawa na ushauri, ambao mkubwa ulikuwa ni kufanya mazoezi zaidi ili kuondoa maumivu.

Lakini pia wapo wengine waliokuwa na changamoto ya maumivu ambao nilipowafikisha kwa Dk Marealle iwe MOI au katika kliniki yake binafsi ya Head2Toe iliyoko Ada Estate, Kinondoni jijini Dar es Salaam mrejesho wao kwa huduma waliyopata ulikuwa chanya.

Tangulia Bro tutakukumbuka daima kwa mchango wako, nasi tuko nyuma yako.