Bryant, Gianna wazikwa kimyakimya Marekani

Thursday February 13 2020

Bryant, Gianna wazikwa kimyakimya Marekani , mpira wa kikapu katika Ligi Kuu ,NBA,Los Angeles Times, Kobe na Gianna,

 

By Matereka Jalilu

Taarifa ambazo hazina shaka zinasema aliyekuwa gwiji wa mpira wa kikapu katika Ligi Kuu ya mchezo huo nchini Marekani (NBA), Kobe Bryant na bintiye Gianna waliofariki dunia kwa ajali ya helikopta binafsi, wameshazikwa katika mazishi ya kifamilia ambayo hayakutangazwa.

Kwa mujibu wa tovuti ya Los Angeles Times, Kobe na Gianna walizikwa Februari 7 katika eneo la Pacific View Memorial Park lililopo Corona Del Mar karibu na mtaa wanaoishi wa Orange County.

Uthibitisho wake umetokana na cheti cha kifo cha Bryant kilichoonyesha sehemu watakapozikwa, ambapo awali ilipangwa wazikwe katika eneo la Westwood Village Memorial Park, lakini ilibadilishwa kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi na familia.

Ujumbe wa mke wa Bryant, Vanessa aliouweka katika mtandao wa kijamii Jumatatu akiugulia maumivu na majonzi ya kuwapoteza wapendwa wake hao uliashiria kufanyika kwa maziko hayo wakati ambapo kumbukumbu maalumu ya kusherehekea maisha yao duniani inatarajiwa kufanyika Februari 24.

Advertisement