Biashara yarejea nyumbani, Ligi Kuu ikiendelea

Muktasari:

Ligi Kuu Bara inarejea tena leo baada ya kusimama kwa siku 10 kupisha kambi ya timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' iliyokuwa ikijiandaa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Burundi na ambao ililala kwa bao 1-0.

Biashara United inarejea kwenye Uwanja wake wa nyumbani Karume, Mara kwa kuikaribisha Ihefu fc leo Jumatano Oktoba 14 huku kocha wa kikosi hicho, Francis Baraza akitamba kuvuna pointi tatu.

Uwanja hupo ulifungiwa na Bodi ya Ligi tangu Septemba 13 ilipoichapa Mwadui bao 1-0 kutokana na ubovu wa sehemu ya kuchezea na vyumba vya kubadilishia nguo lakini juzi Mkurugenzi wa Ufundi wa Shiriksiho la Soka Tanzania (TFF), Oscar Milambo alikwenda kufanya ukaguzi na kuridhika na marekebisho yaliyokuwepo.

Sasa timu hiyo inarejea rasmi kucheza mechi zake za nyumba kwenye uwanja huo baada ya kucheza mechi moja na kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza waliouwa wakiutumia kama uwanja wao wa  nyumbani.

Baraza amesema amefarijika kurtejea tena kwenye uwanja wao wa nyumbani kwani  wamekuwa wakipata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wanaowapa nguvu ya kushinda wachezaji wa kikosi hicho.

"Kama unavyojua msimu uliopita tulikuwa na rekodi bora tunapocheza kwenye uwanmja wetu wa nyumbani sasa baada ya kufungiwa hatukujisikai vizuri kucheza mechi za nyumbani nje ya mkao wetu.

"Tunashukuru uongozi kwa kufanya jitihada kubwa za kuhakikisha wanafanya marekebisho kwa haraka na sasa tumerejea tena tukicheza dhidi ya Ihefu na naamini tutapata ushindi", amesema Baraza.

Biashara United inaikabili Ihefu ambayo hivi karibuni ilimtimua kocha wake Maka Mwalwisi kutokana na matokeo mabaya ya kikosi hicho ambacho kiko nafasi ya pili kutoka mkiani kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara kikiwa na pointi tatu.

Mchezo mwingine leo utazikutanisha KMC itakayoikaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa Uhuru wakati JKT Tanzania itapambana na maafande wenzao wa Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma na Kagera Sugar itakuwa ugenini kupambana na Namungo kwenye uwanja wa Majaliwa Ruangwa Lindi.

Kocha wa JKT Tanzania,Abdallah Mohammed' Bares' amesema  itakuwa moja ya derby kali lakini wanachopambana ni kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo na kuondokana na rekodi mbovu waliyoanza wanapocheza kwenye uwanjani huo.

JKT Tanzania imecheza mechi mbili za ligi msimu huu kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Jamhuri Dodoma na zote imepoteza dhidi ya Dodoma Jiji kwa mabao 2-0 na dhidi ya Simba kwa mabao 4-0.

"Ukiangalia mechi zote mbili tulizocheza kwenye uwanja wetu wa nyumbani tumnepoteza hivyo hatutakubali kupoteza nyingine ya tatu.Najua tunakutana ndugu wawili na mechi itakuwa ngumu sana lakini tumejipanga kupambana kufa na kupona ili kushinda mchezo huo", amesema Bares.

Naye kocha wa Ruvu Shooting, Charles Boniface Mkwasa amesema itakuwa moja ya derby kali  lakini wanachotaka ni ushindi ili kujiimarisha kwenye msimamo wa ligi.