Bellerin anamiliki timu huko England

London, England. Beki wa Arsenal, Hector Bellerin ndiye mtu anayefuatia kwa hisa nyingi kwenye umiliki wa klabu ya League Two, Forest Green Rovers.

Klabu hiyo ambayo imekuwa ikijihusisha sana na mambo ya mazingira kupitia kwenye soka imemvutia Bellerin na hivyo kuamua kuweka pesa zake kwa kuwekeza kwenye timu hiyo ambayo iliwahi kucheza na Arsenal kwenye mechi ya kujiandaa na msimu mpya mwaka 2014.

Rovers inafahamika na Shirikisho la soka duniani (Fifa) na Umoja wa Mataifa kwamba, ni klabu kubwa ya soka inayojihusisha na mambo ya mazingira.

Chini ya mwenyekiti Dale Vince, tajiri wa viwanja anayehamasisha mambo ya mazingira ameifanya timu hiyo kuwa na ushirika na kampuni na watu mbalimbali ambao wamewekeza nguvu kwenye utunzaji wa mazingira.

Hivi karibuni, beki huyo wa Arsenal Bellerin alichagisha pesa kwa ajili ya kupanda miti 60,000 kwenye misimu ya Amazon, Brazil jambo lililowavutia wengi na kuamini kuwa kupitia soka na wanasoka mpango wa kulinda mazingira ya uoto wa asili unaweza kufanikiwa.

Bellerin alisema: “Mara ya kwanza nilipocheza dhidi ya Forest Green Rovers nilichokuwa nikidhani ni klabu inayopatikana mbali sana nje ya London. Niliposikia kile ambacho klabu inafanya, hapo nikapata wazo la kwenda kukutana nao.

“Wakati watu wengi wakiamini hakuna suluhu ya matatizo duniani, kuna Forest Green waliokuja kuonyesha njia mbadala. Nimevutiwa sana kuwa sehemu ya familia ya FGR. Nitasaidia kwa uwezo wangu na kusapoti wanaotaka kuifanya dunia kuwa mahali pazuri.”