Baraza ajipa miezi miwili Biashara

Wednesday September 30 2020

 

By Oliver Albert

Dar es Salaam. Kocha wa Biashara United, Francis Baraza amesema ndani ya miezi miwili ijayo timu hiyo itakuwa moto wa kuotea mbali kwenye Ligi Kuu Bara na haitashikika

Biashara United ambayo msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya tisa, msimu huu imecheza michezo minne, imeshinda miwili na kupoteza mmoja huku ikitoka sare mmoja.

Baraza alisema licha ya kikosi chake kuchelewa kuanza mazoezi ya msimu mpya wa ligi, lakini wana uhakika wa kumaliza katika nafasi za juu zaidi ya msimu uliopita.

“Licha ya wengi kuona tumeanza ligi vizuri, lakini nasema bado ule ubora ninaoutaka timu yangu haijaonyesha na nikuhakikishie ndani ya miezi miwili ijayo tutakuwa tishio.

“Baada ya msimu uliopita kumalizika kuna wachezaji tisa nilikuwa nawahitaji na nilijua kama nigewapata tungekuwa vizuri zaidi, lakini ikashindikana nikawapata watatu tu,” alisema na kuongeza kuwa:

“Ingawa hakuna shida kwani hata hawa nilionao wakichanganyika na wageni wataiwezesha timu hii kufikia malengo msimu huu. Ingawa changamoto niliyoanza nayo ni kwamba, wale wageni bado mpaka sasa nimeshindwa kuwatumia kwa sababu hawajapata vibali vya kazi jambo ambalo wakati mwingine napata wakati mgumu katika baadhi ya mechi kwa sababu wangekuwepo wangesaidia uwanjani.”

Advertisement

 

Advertisement