Bandari yageukia Kombe la shirikisho Afcon

Tuesday July 16 2019

 

By Abdulrahman Sheriff

MOMBASA. BAADA ya kubanduliwa nje ya Mashindano ya Cecafa Kagame Cup huko Rwanda, Bandari FC sasa inapania kufanya mazoezi kabambe kwa ajili ya kujitayarisha kwa mechi ya Kombe la Shirikisho la Bara Afrika.

Naibu Kocha wa Bandari FC, Nassoro Mwakoba aliliambia Mwanaspoti jana Jumatatu asubuhi kabla ya timu hiyo kuondoka Kigali kurudi nyumbani kuwa wanatarajia kucheza mechi ya raundi ya kwanza mkondo wa kwanza hapo Agosti 8 lakini hawajatajiwa wapinzani wao ni nani.

Hata hivyo, Mwakoba alisema mara watakaporudi Mombasa, wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi watakuwa na mapumzikoni kwa kipindi cha wiki moja kabla ya kurudi kuanza matayarisho ya mechi yao ya Confederation Cup.

“Tunaondoka leo kurudi nyumbani ambako tutaweza kupumzika kwa wiki moja halafu tuanze kujiandaa kwa mechi ya kwanza ya Confederation Cup ambapo tutacheza na timu ambayo bado hatujajulishwa ni ipi,” alisema mkufunzi huyo.

Kuhusu mechi zao tatu za Cecafa Kagame Cup, Mwakoba aliwasifu wachezaji wake kwa kucheza kwa kujituma lakini bahati haikuwa yao. “Wanasoka wetu walicheza vizuri sana lakini hatukuwa na bahati kwani walipoteza nafasi nyingi za kushinda,” alisema.

Alidai kukosa uzoefu wa mashindano makubwa ya kiwango hicho pia ilichangia kutoweza kufanya vizuri zaidi akidai wapinzani wao wote walikuwa wenye uzoefu wa mashindano hayo.

Advertisement

“Tulijitahidi sana lakini wenzetu walitumia uzoefu kutufanya tusiendelee mbele.”

Alisema ile kutoshindwa pekee imesaidia sana wachezaji kusoma kutoka kwa wapinzani wao.

 “Tunastahili tuwapongeze wanasoka wetu kwa sababu hatukushindwa hata mchezo mmoja ila tulibanduliwa kwa kuwa wenzetu walishinda mechi moja ama mbili,” alisema.

Advertisement