Bandari FC yapewa somo Caf

Wednesday June 5 2019

 

By Abdulrahman Sheriff

MOMBASA. MABINGWA wapya wa SportPesa Shield, Bandari FC jana imetakiwa ifanye mipango kabambe ya kujitayarisha kwa mashindano ya Caf Confederation Cup ya msimu wa 2019-2020 na inatarajia kucheza mechi ya raundi ya kwanza hapo Agosti.

Hilo ni mojawapo ya mashauri yaliyotolewa na washika dau wa soka wa Mkoa wa Pwani wakati wa kuipongeza timu yao hiyo kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Kariobangi Sharks FC kwenye pambano la fainali lilochezwa Jumamosi na Jumapili.

Kipindi cha kwanza cha mechi hiyo kilichezwa Jumamosi lakini kutokana na mvua kubwa iliyonyesha, kiwanja hakikuwa hali ya kuchezeka na hivyo, dakika 45 za kipindi cha pili zilichezwa juzi Jumapili asubuhi.

Kocha Mkuu wa Skyward Express FC, Mohamed Omar Daddy alisema ni muhimu kwa timu hiyo ya Bandari ianze kupanga mikakati ya kujitayarisha kwa dimba hilo la barani Afrika ili iweze kufanya vizuri.

“Tunataka timu yetu hiyo itambe kwenye mashindano hayo ya Afrika. Tunataka kuweka historia sawa na ile iliyowekwa na Gor Mahia ya kushinda taji hilo. Tunaamini Bandari inaweza lakini lazima ifanye mazoezi ya hali ya juu na kucheza mechi za kujipima nguvu nyingi,” akasema Daddy.

Naye Kocha wa Super Matuga FC, Salim Said Bokande alisema wanajivunia Bandari kushinda ngao hiyo ya SportPesa na akaitaka ifanye bidii kushinda ama kufika mbali kwenye mashindano ya barani Afrika.

Advertisement

“Nawaomba wakuu wa timu hiyo waangazie na kutafuta choipukizi wenye vipaji kutoka sehemu hizi zetu za Mkoa wa Pwani kwani wako wengi na wazuri ambao wanaweza kuipeleka timu yetu hiyo mbali,” akasema Bokande.

Advertisement