Banda: Sina wa kumlaumu kuachwa Taifa Stars -VIDEO

Muktasari:

Banda anayeichezea Baroka FC ya Afrika Kusini alikuwa miongoni mwa wachezaji 32 waliokwenda Misri kujianda na fainali za Mataifa Afrika (AFCON).

Dar es Salaam. Baada ya kuachwa katika kikosi cha Taifa Stars, beki Abdi Banda amesema hana wa kumlaumu kwa sababu timu hiyo ni ya watu wote sasa anakwenda kujipanga ili atakapoitwa kwa mara nyingine awe chaguo namba moja la timu hiyo.

Banda anayeichezea Baroka FC ya Afrika Kusini alikuwa miongoni mwa wachezaji 32 waliokwenda Misri kujianda na fainali za Mataifa Afrika (AFCON).

Beki huyo aliyesumbuliwa na majeruhi kwa muda mrefu pamoja na kukosa namba ya kudumu katika kikosi cha Baroka, amekuwa mmoja wa wachezaji tisa waliotemwa Taifa Stars.

 "Nimekubaliana na uamuzi ya benchi la ufundi  maana timu ya taifa kila mtu anahaki ya kuitumikia nchi yake kama leo nimeachwa  mimi basi kesho nitakuwa mimi," alisema Banda ambaye pia ni mume wa mdogo wa msanii wa Bongo Fleva, Ali Kiba anayeitwa Zabibu Kiba.

"Kikubwa ninachotaka kusema kwa upande wangu sina wa kumlaumu nimiheshimu uamuzi maana nina imani kesho nitarudi tena. Hapa si mwisho wa safari."

Banda alisema anarudi katika klabu yake na kujipanga upya, kuangalia ni wapi hakumridhisha mwalimu ili safari ijayo aweze kuitwa tena akiwa  katika kiwango bora zaidi6.

"Nawapongeza wote waliopata nafasi ya kuiwakilisha nchi na nina imani wataleta heshima tunayoitaka Watanzania,"alimaliza Banda.

Benchi la ufundi chini ya Kocha Emmanuel Amunike, amemwacha Banda pamoja na kiungo mshambuliaji Shiza Kichuya, mshambuliaji Shaban Chilunda, mshambuliaji wa Serengeti Boys Kelvin John na kipa wa timu ya taifa chini ya umri wa miaka 20, Claryo Boniface.

Wengine ambao hawajajumuishwa ni Miraji Athuman, Fred Tangalu, Selemani Salula na David Mwantika.

Kikosi cha wachezaji 23 watakaoiwakilisha Stars kwenye AFCON mwaka huu ni makipa Aishi Manula (Simba), Metacha Mnata (Mbao) na Aron Kalambo (Prisons).

Mabeki ni Hassan Kessy (Nkana FC), Gadiel Michael (Yanga), Mohammed Hussein 'Tshabalala (Simba), Kelvin Yondani (Yanga), Aggrey Morris (Azam) Vincent Philipo (Mbao) na Ally Mtoni 'Sonso' (Lipuli).

Viungo ni Himid Mao (Petrojet), Feisal Salum 'Fei Toto' (Yanga), Yahya Zaydi (Ismailia), Mudathir Yahya (Azam), Frank Domayo (Azam), Farid Musa (Tenerife) na Erasto Nyoni (Simba)

Washambuliaji ni Mbwana Samatta (Genk), John Bocco (Simba), Rashid Mandawa (Huru), Thomas Ulimwengu (JS Saoura), Saimon Msuva (Difaa El Jadida) na Adi Yussuf (Blackpool)