BALAMA fundi atakayeikosa KARIAKOO DERBY Jumapili

Muktasari:
'Bao dhidi ya Simba lilikuwa bao bora kwangu kati ya yote niliyowahi kufunga, hufanyi mazoezi mabao kama yale ila inatokea tu kwa mfungaji'
MWISHONI mwa wiki hii kuna kazi pevu pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kuna wanaume wanapokuwa na jambo lao mambo huwa moto sana. Ndio, zinapokutana Simba na Yanga kwenye ile Kariakoo Derby kila kitu husimama. Lakini, safari hii mechi hiyo ina mzuka zaidi kuwania nafasi ya kucheza fainali ya Azam Sports Federation (ASFC).
Kariakoo Derby ni moja ya michezo inayowagusa mashabiki wengi wa soka nchini, tambo zinaanza nje ya uwanja kuanzia kwa mashabiki, wachezaji na viongozi wakitambiana kuhusu ubora wa vikosi.
Unapotaja dabi za uhakika Afrika na kuzitaja zile za Al Ahly na Zamalek (Misri), Gor Mahia na AFC Leopard (Kenya) basi Tanzania huwezi kuwaacha kuwataja miamba hawa kweye Kariakoo Derby.
Wachezaji wanaona fahari kubwa wanapokuwa kwenye vikosi vya timu hizi mbili na kufanikiwa kucheza dabi hata moja huwa ni kumbukumbu kubwa maishani mwao.
Kiungo fundi wa Yanga, Mapinduzi Balama ni miongoni mwa wachezaji tegemeo kwenye kikosi hicho tangu aliposajili akitokea Alliance FC ya Mwanza.
Katika Kariakoo Derby ya Jumapili, Mapinduzi hatakuwa kwenye kikosi cha Yanga kutokana na kuuguza majeraha. Hivyo, atanguangalia mchezo huu ambao utaamua hatima ya Yanga kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao akiwa jukwaani.
Hata hivyo, tangu alipotua Jangwani msimu ujao, Balama amecheza Derby mbili ambazo zote alitoa mchango mkubwa baada ya kuaminiwa na kupewa nafasi. Lile bao lake la Mwana Ukome kwenye sare ya mabao 2-2 dhidi ya Simba, bado limekuwa kivutio kwa mashabiki wa soka nchini hasa wa Yanga, ambapo Jumapili hatakuwa kwenye eneo la katikati pale Yanga.
NIDHAMU INAMBEBA
“Nilisajiliwa chini ya Mwinyi Zahera, ambaye nashukuru aliniamini na kunipa nafasi kila wakati, kikubwa ni kufuata maelekezo ya yale unayoambiwa na kocha wako.
“Kocha yoyote anapenda mchezaji anayefuata yale anayomwelekeza maana hata alipoondoka na timu kuwa chini ya Mkwasa (Charles) naye alinipa nafasi kama kawaida.
Anasema siku zote amekuwa mtu wa kujifunza na kusikiliza watu wanaomuongoza ndio maana hata leo Kocha, Luc Eyamel naye amekuwa akimpanga kila wakati.
SAFARI BADO
Safari ya soka ya Balama ilianza kuonekana akiwa na Mtwivila FC ya Iringa United ambayo inashiriki Ligi Daraja la Pili (SDL) msimu huu.
Nyota yake ikaonekana na viongozi wa Alliance FC ambao, walimsajili kutokana na uwezo aliouonyesha kwenye moja ya michezo waliyokutana hapo nyuma.
Kiwango chake kilizidi kuwa bora hata aliposajiliwa Alliance FC ambayo inashiriki Ligi Kuu na ndipo mwanzano mwa msimu Yanga ilimsajili kwa mkataba wa miaka mitatu.
Mapinduzi alikuwa mchezaji mpya wa 10 kusajiliwa Yanga SC na wa tatu mzawa baada ya beki Ally Ally kutoka KMC, Abdulaziz Makame kutoka Mafunzo ya Zanzibar.
Wachezaji wageni waliosajiliwa dirisha kubwa ni Sadney Urikhob kutoka Namibia, Lamine Moro (Ghana), Juma Balinya (Uganda), Issa Bigirimana, Patrick Sibomana (Rwanda), Mustapha Seleman (Burundi) na Maybin Kalengo kutoka Zambia.
MALENGO YAKE
Kila binadamu anayehitaji kufikia mafanikio fulani kwenye maisha yake, lazima aweke malengo na mikakati madhubuti kabisa ili kutimiza ndoto zake
‘Malengo yangu siku moja nikacheze soka la kulipwa na sio kuishia hapa nyumbani ndio maana kila ninapopata nafasi ya kucheza huitumia vizuri.
“Ninapofanya vizuri kwenye michezo ninayopata nafasi inanifungulia milango mingine, watu wengi wananiona na hata wale wanaonifuatilia wanakuwa wakivutiwa na kile kizuri ninachokifanya uwanjani,” anasema Balama maarufu kama Kipenseli.
Mpaka sasa Mapinduzi amefunga mabao matatu pekee kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, bao lake la kwanza lilikuwa Januari 4 mwaka huu walipotosahana nguvu na Simba ya mabao 2-2 Uwanja wa Taifa.
Bao lake la pili lilikuwa Februari 5, mwaka huu wakati Yanga ikishinda 2-1 mbele ya Lipuli FC, huku bao lingine la Yanga likifungwa na Bernard Morrison na lile la kufutia machozi kwa Lipuli likifungwa na David Mwasa. Bao la tatu akifunga kwenye ushindi wa bao 1-0 mbele ya Ndanda FC.
KUHUSU KARIAKOO DERBY
Wakati Mapinduzi akifungua kurasa ya mabao msimu huu Januari 4 kwenye sare ya mabao 2-2 dhidi ya Simba, ndio ulikuwa Derby yake ya kwanza.
Bao lingine la Yanga lilifungwa na Mohammed Banka na yale ya Simba yakifungwa na Meddie Kagere kwa penalti pamoja na Deo Kanda.
“Lilikuwa bao bora kwangu kati ya yote niliyowahi kufunga, hufanyi mazoezi mabao kama yale ila inatokea tu kwa mfungaji.
“Moja ya vitu ambavyo naviweka akilini ninapokuwa uwanjani ni kuhakikisha nacheza vizuri kwa kufuata yale ya kocha ikiwa pamoja na kutoa pasi sahihi,” anasema Mapinduzi.
Balama anasema wakati akisajiliwa Yanga hakuwa na shaka, lakini jambo lililomuumiza kichwa ni namna ya kupata namba mbele ya wakongwe.
Bao lake lilikuwa gumzo mtaani karibu wiki nzima kutokana na umbali na namna alivyomtungua, Aishi Manula kipa wa Simba aliyekuwa langoni siku hiyo.
Katika mchezo huo, Simba ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao moja lililofungwa na Kagere kwa mkwaju wa penalti baada ya madhambi aliyofanyiwa na Kelvin Yondani.
Kanda akaongeza bao la pili kabla ya Yanga kuchomoa moja baada lingine.
Balama pia alikuwa kwenye kikosi cha Yanga kilichoilaza Simba bao 1-0 Machi 8, mwaka huu Uwanja wa Taifa kwa bao la Morrison. Katika mchezo huo, Rais John Magufuli alikuwa jukwaani sambamba na Rais wa Caf, Ahmad Ahmad.