Azam yatoa udhamini wa Sh6.3bilioni kwa Kombe la FA, Taifa Stars

Thursday September 12 2019

 

By Charles Abel, Judith Fumbo

Dar es Salaam. Kampuni ya Azam Media na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) leo wamesaini mikataba miwili yenye thamani ya takribani Shilingi 6.3 bilioni kwa haki za matangazo ya Kombe la FA na mechi za timu ya taifa.

Mikataba hiyo miwili imesainiwa leo katika makamo makuu ya Kampuni ya Azam Media yaliyopo Tabata jijini Dares Salaam.

Mkataba wa udhamini wa mashindano ya Kombe la FA ni wa miaka minne na utakuwa na thamani ya Shilingi 4.5 bilioni ambao utaanza msimu huu baada ya ule wa mwanzo kumalizika.

Pia kupitia mkataba mwingine wa udhamini wa timu ya taifa, Azam Media itaipatia TFF kiasi cha Shilingi 100 milioni kwa mwaka kwa mechi ambazo hazipo kwenye kalenda ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) lakini pia kiasi cha Sh35 milioni kwa kila mechi ambayo itakuwa inatambulika na FIFA.

Rais wa TFF, Wallace Karia alisema kusainiwa kwa mikataba hiyo ni ishara tosha ya nia ya dhati ya Azam Media katika kuendeleza soka nchini.

"Mchakato wa kujadili mkataba huu yamepata baraka zote na umepia katika taratibu zote kama katiba ya TFF inavyotaka. Azam wamekuwa washirika wetu kwa asilimia 80 kwani wamekuwa wakitusaidia katika kusukuma mbele mipango yetu mingi ya kimaendeleo," alisema Karia.

Advertisement

Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Tido Mhando alisema kuwa tangu kampuni hiyo ilipoanza kusapoti mchezo wa soka kumekuwa na maendeleo makubwa ya mpira wa miguu hapa Tanzania.

"Kumekuwa na ufanisi mkubwa kwa timu yetu ya taifa na pia tumeona ufanisi mkubwa kwa klabu zetu kwenye mashindano ya kimataifa.

Azam Media tunaamini kwamba tuna mchango wetu katika kupatikana kwa ufanisi na mafanikio hayo," alisema Mhando.

Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao alisema wamejipanga kutatua changamoto za mashindano ya FA.

"Bahati nzuri uongozi wetu umekuwa ukifanya mambo kwa uwazi mkubwa na sisi pamoja na wenzetu wa Azam Media tumekaa chini kujadili changamoto zilizojitokeza msimu uliopita na niwahakikishie kwamba zitapungua kwa kiasi kikubwa msimu ujao," alisema Kidao.

Mkurugenzi wa michezo wa Azam Media, Patrick Kahemele alisema kuwa kampuni hiyo ina imani kubwa kuwa mikataba hiyo italeta tija kwa soka la Tanzania.

"Tunaamini timu ya taifa ikipata idadi kubwa ya mechi za kirafiki, itatusaidia kupandisha kiwango," alisisitiza Kahemele

Advertisement