Azam FC waiwaza Coastal Union, vikosi viwili....

Muktasari:

Kikosi cha Azam FC, kimetamba kuimaliza Coastal Union ya Tanga watakayocheza nayo Jumamisi hii, lakini wameweka wazi timu yao ina vikosi viwili matata.

AZAM FC, wanaendelea na maandalizi kuhakikisha wanalipiza kisasi kwa Coastal Union ya Tanga, watakayocheza nayo kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Azam FC na wageni wao hao, watacheza mchezo huo saa 10: 00 jioni, ukiwa ni mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu Bara, ambapo raundi ya kwanza kufungwa bao 1-0 jijini Tanga.
Kocha wa Azam FC,  Aristica Cioaba, ameweka wazi kuwa kikosi chake kiko vizuri tayari kwa mchezo huo.
"Mechi ngumu, inahitaji ufundi wa hali ya juu kwa sababu Coastal ni timu nzuri na imekuwa na matokeo mazuri katika mechi zao. Najua aina gani ya mchezo wanaocheza hivyo nimejiandaa kuwadhibiti na kushinda,"alisema Cioba.

VIKOSI VIWILI KABAMBE
Afisa Habari wa Azam FC, Jafar Idd ametamba timu yao kuwa na vikosi viwili kabambe.
"Kwa sasa timu yetu haina majeruhi jambo linalofanya tuwe na vikosi viwili vizuri kabisa. Hii inampa urahisi Kocha Cioba kufanya uchaguzi wa wachezaji anaopenda kuwatumia kulingana na mchezo husika,"alisema Jafar.
"Pia, ni kama tuna timu mbili kwa sasa, kuna wakati unaona sehemu ya wachezaji wanacheza na wakati mwingine huwaoni, wanakuwa wanaandaliwa kwa ajili ya michezo mingine."