Anguko la Aussems Simba SC lilianzia hapa tu

Muktasari:

Hapana, Patrick Aussems amekuwa mwathirika wa mambo kadhaa ambayo inabidi yatafutiwe dawa mapema, la sivyo klabu itakwama.

SIMBA SC wametangaza kuachana na kocha wao, Patrick Aussems, wakisema ameshindwa kufikia malengo waliyokubaliana awali wakati akisaini mkataba klabuni hapo.

Wanasema moja ya masharti yalikuwa kushiriki mashindano ya kimataifa, ambayo wametolewa katika raundi ya awali ya mchujo.

Unaweza ukajiuliza, huyu si ndiyo kocha aliyevuka malengo msimu uliopita?

Malengo yao yalikuwa kufika hatua ya makundi, lakini akawafikisha robo fainali. Hawajui kwamba kwenye biashara kuna siku za faida na za hasara pia?

Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Mo, kama mfanyabiashara mkubwa, anajua sana hilo...unadhani bodi ni wajinga?

Hapana, Patrick Aussems amekuwa mwathirika wa mambo kadhaa ambayo inabidi yatafutiwe dawa mapema, la sivyo klabu itakwama.

1. MENEJA PATRICK RWEYEMAMU

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, hakuwa akielewana na Aussems tangu siku ya kwanza walipotambulishwa kwamba, watafanya kazi pamoja.

Maisha yao yote yamekuwa ya kusumbuana na kutafuatiana kufeli ili mmoja aharibikiwe.

Mara nyingi amekuwa akilumbana na kocha kuhusu mambo ya kiufundi ya timu.

Mfano ni tukio la Novemba 3, 2019, kwenye mchezo wa VPL dhidi ya Mbeya City.

Meneja alibishana na kocha kuhusu mabadiliko katika dakika ya 79 pale Aussems alipotaka kumuingiza Deo Kanda kuchukua nafasi ya Ibrahim Ajibu, huku Rweyemamu akitaka aingie Dilunga.

Aussems akishinda matakwa yake na Kanda akaingia. Mungu si Athuman, Kanda akafunga bao. Aussems akamgeukia Rweyemamu kwenye benchi na kumbania pua huku akisema ‘Dilunga Dilunga’, kama ishara ya kumbeza kwa yale malumbano.

Meneja anabishana vipi na kocha kwenye suala la mabadiliko ya mchezaji? Ni bora hata angekuwa kocha msaidizi ingeeleweka kidogo.

Rweyemamu pia amekuwa akilumbana na kocha kuhusu kuwaweka benchi Said Ndemla, Ibrahim Ajibu na Beno Kakolanya, akiamini katika nafasi zao kwa sasa wako vizuri kuliko wanaopewa nafasi.

“Mlevi wa mwaka jana si sawa na mlevi wa mwaka huu,” ni kauli yake, akimzungumzia Clatous Chama.

2. DENNIS KITAMBI

Mahojiano yake ya Novemba 27 kwamba aliitwa na Afisa Mtendaji Mkuu na kuambiwa atakaimu nafasi ya kocha mkuu kwa sababu Aussems amesimamishwa, ni ya kufikirisha kidogo.

Hii ni kutokana na mfululizo wa matukio yanayomkuta bwana huyu.

Safari yake ya ukocha ilianzia Ndanda FC, akiwa msaidizi wa Amri Said, 2013/14 wakati wa harakati zao za kupanda Ligi Kuu.

Lakini baadaye, Said akaondoka na kumuacha Kitambi kama kaimu kocha mkuu...akaisaidia Ndanda kupanda 2014, lakini hakudumu nayo kwenye ligi.

Machi 2015, Kitambi akaajiriwa na Azam FC kuwa msaidizi wa kocha raia wa Uganda, George ‘Best Nsimbe’ lakini mwisho wa msimu, Nsimbe akaondoka...yeye akabaki.

Akawa msaidizi wa Stewart Hall ambaye waliondoka naye kwenda AFC Leopards ya Kenya 2016. Huko, Hall akaondoka, yeye akabaki kama kaimu kocha mkuu na akaja na timu hiyo Dar es Salaam, kwenye mashindano ya SportPesa 2017. Unakumbuka?

Na sasa imemtokea tena akiwa Simba SC. Kitambi amekuwa na bahati mbaya ya makocha wakuu kuondoka kisha yeye akabaki na kupewa timu.

3. KAZI NA DAWA

Moja ya sababu zilizotajwa katika kuhalalisha ‘kuliwa kichwa’ kwa Aussems ni kuchangia kwake kushuka viwango vya baadhi ya wachezaji.

Tuhuma hii hailengi katika mbinu zake za ufundishaji, bali maisha yake kambini.

Aussems amekuwa kocha anayependa kijiachia sana baada ya kazi. Vijana wa mjini wanasema kazi na bata. Ndio bata batani.

Inasemekana hufanya starehe mbele ya wachezaji na kuwasababisha watamani kufanya kama yeye, na ndo kisa cha kuharibikiwa.

Wachezaji kama Jonas Mkude, Chama na Wawa, wamekuwa marafiki zake wakubwa kwenye mitoko ya ‘mabata’.

Mbaya zaidi, kocha huyo alikuwa haambiwi kitu kuhusu wachezaji hao ambao, wamekuwa wakilalamikiwa kushuka viwango.

Chama na Mkude waliikosa safari ya Kanda ya Ziwa kwa sababu ya ‘kujiachia’ sana usiku wa safari kiasi cha kuchelewa kuamka na kushindwa kusafiri.

Mbaya zaidi, hawakulala kambini...walikuwa kwenye bata zao. Lakini kocha hachukui hatua kali dhidi yao kwa sababu wanachokifanya, yeye hufanya nao.

4. MPASUKO KWENYE TIMU

Wachezaji waliosajiliwa na Simba kutoka Azam FC; nahodha John Bocco, kipa Aishi Manula, kiraka Erasto Nyoni na Shomary Kapombe, wamekuwa wakijitenga sana na wenzao.

Hata safari za uwanjani kutokea kambini, mara nyingi hawapandi basi la timu...wao huenda na magari yao binafsi.

Hali hii imekuwa ikifumbiwa macho na kocha Aussems kiasi cha wachezaji wengine kutokuwa na furaha nayo na kulalamika kwamba ‘hawa jamaa wanaleta uazamu wao hapa’.

5. MTENDAJI MKUU MAZINGISA

Inasemekana tangu siku ya kwanza, Mazingisa alitaka kuleta watu wake kwenye benchi la ufundi la Simba.

Aussems alilishtukia hilo na alishawahi kumwambia msaidizi wake, Dennis Kitambi, kwamba ‘hapa hatuna maisha marefu’.

Mazingisa anataka kuwaweka watu anaowaamini ili wamfanyie kazi yake, badala ya kina Aussems ambao waliiongoza timu kupata mafanikio makubwa msimu uliopita.

Katika kufanikisha mpango wake, amekuwa akitumia ombwe la kimfumo ndani ya klabu hiyo na kutengeneza ‘jambo lake’.

Naye baada ya kuona watu hawa hawezi kufanya nao kazi, akakataa kuwapa ushirikiano wowote, akawa anawasiliana na ‘Boss’ Mo moja kwa moja.

Bwana Mazingisa akapata sababu kwamba, ‘ananidharau mimi Boss wake, kwa hiyo siwezi kufanya naye kazi’.

Boss kubwa Mo akaona kuna mashiko kwa sababu wakati mwingine anaelezwa mambo ambayo yalitakiwa yaishie kwa CEO. Akaona ‘kocha huyu ana shida’...

Ni mjumuiko wa mambo hayo na mengine mengi madogo madogo ndiyo yaliyokamilisha safari ya Patrick Aussems kuondoka Simba SC.

Lakini, kuondoka kwake lazima kuwe somo kwa Simba.