Alliance FC yatembeza rungu

Wednesday November 6 2019

Alliance FC- yatembeza- rungu-mbeya city-kadi nyekundu-michezo blog-mwanasport-mwanaspotiGazeti-MwanaspotiSoka-

Kipa wa Alliance FC,John Mwanda (wa tano kutoka kulia mstari wa mbele) akiwaongoza wachezaji wenzake kupasha katika moja ya mechi za Ligi Kuu msimu huu.Mlinda mlango huyo amepigwa faini ya Sh200,000 na klabu yake kwa kitendo cha kuonyeshwa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Mbeya City.Picha |Masoud  Masasi 

By Saddam Sadick,Mwanza


KAMATI ya nidhamu ya Alliance FC imewapiga faini wachezaji wawili waliopewa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Mbeya City.

Wachezaji hao ni kipa John Mwanda na nahodha Israel Patrick.

Mchezo huo ulipigwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Nyamagana, ambapo wachezaji hao walionyesha vitendo visivyo vya kiungwana kwa wenzao na kusababisha mwamuzi Shomari Lawi kuwaonyesha kadi nyekundu kila mmoja.

Katika mechi hiyo, Mwanda alionekana kumchezea rafu straika wa Mbeya City, George Chota huku Patrick akionyesha kumshika sehemu nyeti mchezaji Idd Gomba na kusababisha Alliance kumaliza mpambano wakiwa pungufu.

Makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Stephano Nyaitati alisema katika kuhakikisha nidhamu inatawala kamati ilikaa juzi na kuamua wachezaji hao kulipa faini kulingana na makosa husika.

Alisema Patrick aliamuriwa kulipa faini ya Sh250,000 huku Mwanda akitakiwa kulipa Sh200,000 na hiyo ni kwa mujibu wa kanuni za klabu kwa wachezaji.

Advertisement

“Kamati imekaa leo (juzi) na kuamua wachezaji hao kulipa faini hizo, hii ni kwa mujibu wa kanuni za klabu katika hali ya kulinda nidhamu,” alisema Nyaitati.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa klabu inaendelea kulaani vitendo vya utovu wa nidhamu vilivyoonyeshwa na nyota wake, huku akisisitiza kuwa hawatasita kuchukua hatua pindi hali hiyo itakapojitokeza. “Tumejipanga kulinda na kutetea nidhamu hata wale wengine wataendelea kutumikia adhabu hadi mwezi uishe,” alisema.

Advertisement