Ajali ya moto yaua mchezaji, wengine wawili wanusurika

Sunday August 11 2019

 

By IMANI MAKONGORO

AJALI ya moto iliyoua zaidi ya watu 60 mjini Morogoro imewagusa watu wa soka baada ya kubainika mmoja ya wachezaji wa Moro Kids naye amefariki katika mkasa huo, huku wengine wawili ambao ni ni wanasoka wakiachwa na majeraha mabaya.

Mchezaji aliyepoteza uhai kwenye tukio lililotokea asubuhi ya jana eneo la Msamvu, mjini humo ni Simon Dickson anayeichezea timu ya Kituo hicho cha kukuza na kulea vipaji kilichopo mjini humo baada ya lori la kubeba mafuta kupinduka na kulipuka moto.

Mbali na kifo hicho, wachezaji wawili wa timu ya Burkina Faso inayoshiriki Ligi Daraja la Pili na inayonolewa na nyota wa zamanio wa Simba, Ulimboka Mwakingwe wamenusurika kifo katika ajali hiyo na  hali zao ni mbaya.

Wachezaji hao ni Dachi Kombo ambaye inaelezwa ameungua mwili mzima na Mudy Nyeto ambaye amungua kuanzia kiunoni mpaka miguuni.

Kocha wa Kituo cha Moro Kids, Abdallah Unika alisema, kituo chao kimepata pigo kutokana na msiba wa mchezaji huyo.

"Ni mchezaji wangu ambaye namfundisha kwenye kituo cha Moro Kids, ni msiba mzito kwa kweli," alisema kocha huyo kwa masikitiko.

Advertisement

Akizungumzia mazingira ya ajali hiyo, kocha Unika alisema imewahusisha watu ambao pia walikuwa wakipita na wengine wakiendelea na shughuli zao pembeni ya barabara.

"Nimeishuhudia wakati inatokea, eneo lile lina pilika pilika za watu, wapo wanaouza mitumba, wengine chakula njiani, na jana (siku ya ajali) kulikuwa na maonyesho ya nane nane hivyo pilikapilika za watu kwenda kumalizia nane nane ilikuwa kubwa wakitokea mjini na wengine kutoka nane nane kurudi mjini," alisema.

Advertisement