Tuzo Ligi Kuu zawakosha mastaa

Muktasari:

BAADHI ya wachezaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wamezungumzia uwepo wao katika kinyang'anyiro cha kuwania tuzo ya mchezaji bora wa msimu uliofikia tamati wikiendi iliyopita 2019/2020.

BAADHI ya wachezaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wamezungumzia uwepo wao katika kinyang'anyiro cha kuwania tuzo ya mchezaji bora wa msimu uliofikia tamati wikiendi iliyopita 2019/2020.

Jana Bodi ya Ligi Kuu ilitangaza majina ya nyota 30 kutoka katika timu mbalimbali za Ligi kuu ambao watawania tuzo hiyo, itakayotolewa Agost 7 mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.

Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti, wachezaji hao wamesema kuwa kitendo cha kuingia katika kundi la nyota 30 bora kimewapa faraja.

"Mimi kama mchezaji huu mchezo wa mpira ni jambo la kumshukuru Mungu, na hao walionichagua na kuniona nafaa kuingia katika mchakato huo, kwangu mimi nasema Mungu mkubwa, mpaka apatikane mmoja sio jambo dogo na inazidi kunipa moyo na kunifanya nijitume zaidi," alisema beki wa Kagera Sugar, David Luhende

Kiungo wa Yanga, Feisal Salum 'Fei Toto alisema hatua aliyofika hadi sasa  ni kubwa na anamshukuru Mungu kwa hilo.

"Ni mipango ya Mungu kuwa miongoni mwa wachezaji 30, sio jambo dogo wala jepesi, namshukuru sana Mungu wachezaji tuko wengi lakini kwa nini mimi jibu analo Mungu," alisema Fei Toto.

Naye mshambuliaji wa Namungo FC, Blaise Bigirimana alisema, "imi kitendo tu cha kutangazwa katika hao 30, kwangu ni faraja na ni hatua nyingine tena katika maisha yangu ya mpira, pia nawashukuru wachezaji wenzangu kwa ushirikiano wao mpaka nikaonekana bora,"

Mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Marcel Kaheza amesema kuwa jambo lililotokea ni kubwa na la thamani kwa upande wake

 

"Sio jambo dogo hilo, kwangu mimi ni kitu kikubwa sana, japokuwa ndio kwanza kumekucha kati ya 30 anatakiwa mmoja, kwa atakayepata atakuwa amestahili ni kama ambavyo waliochagua walituona tunafaa na mimi nikiwemo, kwangu mimi napata deni sasa," alisema Kaheza.

 

Wakati huo huo Mchezaji wa zamani wa Yanga ambaye pia ni mchambuzi wa soka Ally Mayai ameiambia Mwanaspoti kuwa, ili mchezaji awe bora katika msimu inategemea na aina ya mchango alioutoa kwa timu na ukaisaidia timu yake.

 

"Mchezaji bora anaangaliwa aliyeisaidia timu na mchango wake ukawa na matokeo.

Mchezaji bora hawezi kutoka katika timu ambayo haijapata matokeo, au timu ambayo imenusurika kushuka faraja, natolea mfano timu kama KMC haina mchezaji hata mmoja na hali yao ya mwisho iliwafanya washindwe kuingia katika kinyang'anyiro.

David Luhende wa Kagera amecheza mechi nyingi sana katika timu yake, na hajapata majeruhi anafaa kabisa kuwemo katika shindano, lakini hakuna ubishi wowote Simba ina nafasi kubwa wachezaji wake ya mchezaji wa tuzo hiyo kutoka kwao na ndio maana wako wengi kwa kuwa mchango wa waliotajwa ulisaidia timu,"amesema Mayai.

Wachezaji wanaowania tuzo hiyo ni Shomari Kapombe, John Bocco, Meddie Kagere, Clatous Chama, Francis Kahatta, Jonas Mkude, Luiz Miquissone na Aish Manula (Wote kutoka Simba), Feisal Salum, Mapinduzi Balama, Deus Kaseke, David Molinga na Juma Abdul (Yanga)Birigimana Blaise, Lucas Kikoti na Reliants Lusajo (kutoka Namungo), David Luhende, Awesu Awesu, Yusuph Mhilu ( Kagera Sugar), Martin Kigi (Alliance), Daluwesh Saliboka (Lipuli) na Marcel Kaheza (Polisi Tanzania).

Pia wapo Nico Wadada, Idd Nado na Obrey Chirwa ( wote kutoka Azam), Abdulmajid Mangalo, Daniel mgore (Biashara United), Ayoub Lyanga na Bakar Mwamnyeto (Coastal Union) na Waziri Junior (Mbao Fc).