Beki Yanga aitangazia vita Kagera Sugar

Tuesday July 7 2020

 

By James Mlaga

Beki na nahodha msaidizi wa Yanga, Juma Abdul ametamba kuwa timu yake itaibuka na ushindi dhidi ya Kagera Sugar katika pambano lao keshokutwa mkoani Kagera licha ya ubora wa wapinzani wao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Abdul alisema anafahamu Kagera Sugar watacheza kwa nguvu mechi hiyo kwa ajili ya kulipa kisasi baada ya kufungwa na Yanga katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam lakini wao watahakikisha hilo halitokei.

"Malengo yetu kesho ni kupata pointi tatu, tukishinda tutapata nguvu zaidi ya kupambana na Simba. Mechi itakuwa ngumu maana Kagera Sugar siku zote huwa wanaleta ushindani hasa wakutanapo na timu kubwa ila sisi tutapambana," amesema Abdul.

Abdul amesema kuwa wachezaji wote wa Yanga wako tayari kwa mchezo huo na yeyote ambaye atapangwa atapambana kikamilifu kuhakikisha timu inapata ushindi.

"Kama ujuavyo bosi wetu ni kocha.Nikipata nafasi ya kucheza nitapambana, lakini pia mchezaji yoyote akipata nafasi ya kuanza pia naamini atafanya hivyo. Mashabiki wetu waje kutupa hamasa, hatuwezi kuwaangusha," amesema beki huyo.

Yanga wanaingia katika mchezo huo wakiwa na takwimu nzuri za kushinda mbele ya Kagera Sugar kulinganisha na wenyeji wao.

Advertisement

Takwimu zinaonyesha kuwa katika michezo 10 iliyopita ambayo imekutanisha timu hizo katika mashindano mbalimbali, Yanga imeibuka na ushindi mara tisa (9) huku Kagera wakipata ushindi mara moja.

Lakini pia hata katika mechi 10 zilizopita za Ligi Kuu zilizokutanisha timu hizo katika Uwanja wa Kaitaba, Yanga wameshinda saba (7) huku Kagera wakishinda tatu (3) tu.

Advertisement