Morrison arudi kibabe Yanga

Thursday July 2 2020

 

By Thobias Sebastian

Dar es Salaam. Licha ya kuwepo mvutano kati ya Uongozi wa Yanga na mchezaji  Bernard Morrison, kocha wa timu hiyo,  Luc Eymael amemtaka mchezaji huyu kurudi mazoezini na  kama atafanya vizuri amepanga kumtumia katika mechi ya nusu fainali ya kombe la Shirikisho la Azam (ASFA), itakayochezwa Julai 12 kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Eymael alisema mchezaji huyo bado ana mkataba na Yanga hivyo anatakiwa kuwepo mazoezini kama ilivyo kwa wenzake na masuala yake ya utovu wa nidhamu yatashughulikiwa na uongozi.

"Morrison ni mchezaji wa Yanga kama walivyo wengine wote waliokuwa kwenye kikosi kwa sasa na ambao watakuwa katika hali nzuri ya ushindani pindi ambapo tutaanza maandalizi ya kucheza na Simba watapata nafasi ya kutumika na hakuna suala la kuangalia ukubwa wala jina la mchezaji .

Habari nyingine njema kwetu ni kurejea kwa nahodha, Papy Tshishimbi ambaye licha ya kuendelea na vipimo mbalimbali pamoja na matibabu ya taratibu ameanza mazoezi mepesi ambayo yanatia matumaini makubwa hatarejea uwanjani haraka," alisema Eymael

Eymael alisema kuna uwezekano finyu kwa Tshishimbi kucheza michezo inayofuata ya Yanga kwenye Ligi Kuu lakini anaweza kucheza Kombe la Azam Sports Federation.

"Tshishimbi namuona anaweza kushindwa kutumika katika hizi mechi mbili za ligi dhidi ya Kagera Sugar na Biashara United na kama atakuwa na maendeleo mazuri kama ambavyo yalivyo wakati huu naweza kumtumia katika mechi na Simba," anasema Eymael

Advertisement

Yanga na Simba zitakutana katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam itakayochezwa Julai 12 kwenye Uwanja wa Taifa jijini na mshindi wa mechi hiyo atakutana na mshindi wa mchezo baina ya Sahare All Stars na Namungo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga, Julai 11.

Advertisement