Miaka 10 ya Bongo Star Search kulindima mikoa mitano Tanzania

Tuesday September 17 2019

Miaka 10, Bongo Star Search, kulindima Dar, Arusha, Dodoma, Mbeya, Tanzania, Mwanaspoti

 

By Rhobi Chacha

Dar es Salaam. Msimu wa mpya wa shindano la kusaka vipaji la Bongo Star Search (BSS) utafanyika katika mikoa mitano na usaili kufanyika kuanzia mkoani Arusha Septemba 28 na 29, na kuhitimishwa jijini Dar es Salaam Oktoba 23 hadi 26, mwaka huu ikiwa na kauli mbiu ya shindano la BSS ni  "Kinyumbani zaidi ngoma inayeya".

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Septemba 17, 2019, Mkurugenzi Mkuu wa Benchmark Productions na Jaji Mkuu wa BSS, Rita Poulsen alisema ujio wa msimu wa kumi huku akitaja ongezeko la mikoa ambayo itafikiwa na usaili wa shindano hilo.

“Nina furaha kwa sababu ni ‘anniversary’ ya miaka 10 ya Bongo Star Search, najivunia vipaji ambavyo tumevileta mbele ya Watanzania na kuwapa nafasi vijana hao wa kitanzania kuendeleza maisha ya kimuziki na wengine kufanikiwa nje ya muziki pia.

“Habari njema kwa Watanzania ni kwamba tumeongeza idadi ya mikoa ambayo itafikiwa na usaili wa BSS mwaka huu ni Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma na Dar es Salaam,” alisema Rita.

Meneja Masoko StarTimes Tanzania, David Malisa amesema Kampuni ya Star Media (T) Ltd kupitia chapa yake ya StarTimes itaonyesha mchakato mzima wa BSS kupitia chaneli ya StarTimes Swahili.

“Huu unakuwa ni msimu wa pili mfululizo kwa shindano hilo kuruka kupitia chaneli hiyo, sisi tunawaamini Watanzania kama wao walivyotuamini na kuchagua kutumia huduma na bidhaa zetu, na kwa kuzingatia hilo tunaendelea kubeba uhalisia wa jamii ya kitanzania na aina ya burudani ambayo wamekuwa wakiifurahia kwa miaka 10 sasa, nazungumzia BSS na vimbwanga vyake.

Advertisement

“StarTimes tunajali uchumi wa kila Mtanzania na nadhani ni dhahiri kupitia bei zetu hivyo nitangaze rasmi kwamba Bongo Star Search mwaka huu itapatikana kuanzia kifurushi cha NYOTA ambacho gharama yake ni Sh 8,000 tu kwa watumiaji wa kisimbuzi cha antena na Sh 11,000 tu kwa watumiaji wa kisimbuzi cha Dish,” alisema.

Advertisement