Wanyarwanda kuichezesha Azam, Triangle United

Muktasari:

Mshindi wa mechi mbili baina ya Azam FC na Triangle atatinga hatua ya mwisho ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo itahusisha pia timu 16 zitakazotolewa kwenye hatua ya kwanza ya  Ligi ya Mabingwa Afrika

Dar es Salaam.Wakati wapinzani wa Azam kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Triangle United kutoka Zimbabwe wakibadili ratiba ya ujio wao, mwamuzi kutoka Rwanda, Ruzindana Nsoro ndiye atashika kipyenga kuchezesha mechi baina ya timu hizo, Jumapili mwishoni mwa wiki hii.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffary Iddi, alisema kuwa Mwamuzi huyo ambaye alipata beji ya kimataifa ya uamuzi kutoka Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), mwaka 2016, atasimama katikati akisaidiwa na wenzake watatu kutoka nchini humo huku Kamisaa wa mchezo akipangwa kutoka Uganda.

"Ndugu zangu waandishi wa habari ni kwamba bado tupo katika maandalizi yetu ya mchezo wa kimataifa kati ya Azam na timu ya Triangle kutoka kule Zimbabwe. Lakini maandalizi hayo yakiwa yanaendelea, kesho tunatarajia kuwapokea waamuzi kutoka nchini Rwanda.

Waamuzi hao ni Ndagijamana Theogene, John Karangwa na Nsoro Ruzindana hawa ni waamuzi ambao ni watatu kwa maana ya mwamuzi wa akiba namba moja, mwamuzi msaidizi namba mbili na refa wa kati lakini vilevile yupo mwamuzi wa mezani ambaye ni Jean Claude Ishimwe wote kutoka Rwanda," alisema Iddi

Katika hatua nyingine, msimamizi wa mechi hiyo, Mike Letti kutoka Uganda anatarajiwa kutua leo huku Triangle ambao walitegemewa kuwasili nchini jana, wakipanga kuja Jumamosi

Lakini kesho hiyohiyo itakuwa ni siku kwetu ya kuzidi kupokea wageni zaidi. Tunatarajia kumpokea msimamizi wa mchezo au kamisaa kutoka Uganda ambaye anaitwa Mike Letti.

Niseme tu kwamba jana tulikuwa tunatarajia vilevile kuwapokea timu ya Triangle kwa kesho lakini wao wamebadilisha utaratibu na kwamba watafika siku ya Jumamosi na Jumapili wataingia uwanjani lakini bado hawajasema watafika na msafara wa watu wangapi," aliongeza Iddi