Yanga yatoa msaada wa jezi Toto Africans

Monday September 9 2019

Yanga yatoa, msaada wa jezi, Toto Africans, Tanzania, mwanaspoti, Michezo, Mwanza

 

By Saddam Sadick

Mwanza.Wakati Toto Africans ikijiandaa kushuka uwanjani kesho Jumanne kuwakabili Yanga katika mchezo wa kirafiki, viongozi wa Yanga tawi la Mwanza wameikabidhi timu hiyo jezi kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Daraja la pili.

Yanga itawavaa Toto 'Wanakishamapanda' kesho ikiwa ni mechi yake ya pili jiji hapa kujiweka tayari na mechi yake ya Ligi ya mabingwa Afrika itakayopigwa Jumamosi ya wiki hii dhidi ya Zesco.

Akikabidhi vifaa hivyo, Mwenyekiti wa matawi ya Yanga Mwanza, Saleh Akida amesema wameamua kuisapoti timu hiyo ili kuiwezesha kufanya vizuri katika Ligi yao.

"Thamani ya vifaa ni Sh 500,000 ikiwa ni jezi na soksi, lengo ni kuisapoti timu hii yenye historia kubwa nchini, wadau wengine wajitokeze kuipa nguvu, tumejipanga sisi Yanga Mwanza kupitia kampuni yetu ya Kabunda Security kutoa kile tulichonacho," alisema Akida.

Mwenyekiti wa Toto Africans, Rajabu Mbaramwezi alisema msaada huo ni muhimu kwao kwani awali walikuwa na pea moja, hivyo kwa sasa imeongezeka nyingine ambayo itawasaidia.

"Niwashukuru sana Yanga kwa msaada huu, hakika inatupa nguvu na kutambua tuko nao pamoja niombe tuendelee kushirikiana, lakini niwakaribishe wadau wengine kutusapoti" amesema Mbaramwezi.

Advertisement

Advertisement